Michezo

Kipruto alivyomtoa jasho Kipchoge katika Tokyo Marathon

March 4th, 2024 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

BENSON Kipruto aliendeleza rekodi nzuri dhidi ya Mkenya mwenzake Eliud Kipchoge hadi marathon tatu baada ya kutawala mbio za Tokyo Marathon nchini Japan, Jumapili.

Katika raundi hiyo ya kwanza ya Marathon Kuu Duniani (WMM), ambayo ilivutia zaidi ya washiriki 37,000, bingwa wa Boston Marathon 2021 na Chicago Marathon 2022 Kipruto alikata utepe wa kwanza kwa saa 2:02:16.

Alimtoka kabisa Mkenya mwenzake Timothy Kiplagat katika kilomita ya 35 na kushinda jijini Tokyo kwa muda huo wake bora mpya.
Alikuwa na muda bora wa 2:04:02 kutoka Chicago Marathon 2023 kumaanisha aliuimarisha kwa dakika moja na sekunde 46.

Kipruto, 32, pia alifuta rekodi ya Tokyo Marathon ya 2:02:40 ambayo Kipchoge aliweka mwaka 2022 akishinda makala ya 2021.

takumbukwa kuwa Kipruto alimaliza mbele ya Kipchoge katika London Marathon mwaka 2020 na pia Boston Marathon mwaka 2023.

Kipruto alifuatwa kwa karibu na Kiplagat na Mkenya Vincent Ngetich walioimarisha muda yao kutoka 2:03:50 na 2:03:13 hadi 2:02:55 na 2:04:18, mtawalia.

“Mbio zilikuwa nzuri. Nafurahia kuweka rekodi mpya ya Tokyo Marathon,” alisema Kipruto baada ya ushindi.

Kipchoge anayeshikilia muda bora duniani kwa watimkaji walio hai wa saa 2:01:09 kufuatia kifo cha mshikilizi wa rekodi ya dunia Kelvin Kiptum (2:00:35) hapo Februari 11, alitarajiwa kufanya vyema.

Hata hivyo, Kipchoge, 39, ambaye ni bingwa mara mbili wa Olimpiki na ameshinda WMM mara tano, aliachwa katika kilomita ya 20 na kuambulia nafasi ya 10 kwa saa 2:06:50.

Ni marathon ya pili Kipchoge hajashinda kutoka 19 ambazo ameshiriki tangu aanze mashindano ya 42km mwaka 2013 naye Kipruto sasa ana ushindi mara tatu katika marathon saba kubwa.

Juhudi za bingwa wa Tokyo Marathon 2023 Rosemary Wanjiru kutetea taji, zilizimwa akiridhika na nafasi ya pili kwa 2:16:14.

Hata hivyo, mkazi huyo wa Japan aliimarisha muda wake bora kwa sekunde 14. Alimaliza katikati ya Waethiopia Sutume Kebede (2:15:55) na Amane Beriso (2:16:58), mtawalia. Mholanzi Sifan Hassan aliyepigiwa upatu kuibuka malkia, alikamata nafasi ya nne.

Watimkaji waliokamilisha ndani ya tano-bora jijini Tokyo wanatarajiwa kutuzwa Sh7.2 milioni, Sh3.6m, Sh1.8m, Sh1.0m na Sh720,116, mtawalia.

Tano-bora pia walitia kapuni pointi 25, 16, tisa, nne na moja kwenye WMM inayojumuisha pia raundi ya Boston (Aprili 15), London (Aprili 21), Berlin (Septemba 29), Chicago (Oktoba 13) na New York (Novemba 3).

Kila marathon ya mwaka wa Olimpiki pia hujumuishwa kwenye ligi hiyo ambayo tano-bora wanapokea kati ya Sh7.2m na Sh0.7m.

Kipruto, Kiplagat, Ngetich, Kipchoge na Wanjiru wako katika timu ya taifa itakayoshiriki Olimpiki baadaye mwaka huu jijini Paris, Ufaransa.