Michezo

Kipruto asihi AK izoeshe wanariadha kufanya mazoezi katika hali mbalimbali za hewa

October 20th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

BINGWA wa zamani wa Toronto Marathon, Bernard Kipruto, hatashiriki mbio zozote mwaka huu baada ya kupata jeraha la paja wakati wa kivumbi cha London Marathon mnamo Oktoba 4, 2020.

Kipruto aliambulia nafasi ya saba jijini London, nambari moja mbele ya bingwa wa dunia na mshikilizi wa rekodi ya dunia, Eliud Kipchoge, aliyetupwa hadi nafasi ya nane baada ya kupata tatizo la sikio katika hatua ya kilomita 25.

“Nilikuwa nimejiandaa vya kutosha kwa mbio hizo na azma yangu ilikuwa kuwa miongoni mwa washindi watatu bora. Hata hivyo, jeraha lilinitatiza kufikia hatua ya kilomita 30 na kasi yangu ikapungua kabisa,” akasema Kipruto.

Mbali na jeraha, Kipruto alilalamikia pia hali mbovu ya hewa jijini London kuwa kiini cha kutotamba kwake katika mbio hizo zilizotawaliwa na Mwethiopia Shura Kitata Tola kwa muda wa saa 2:05:41.

“Itakuwa muhimu kwa Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) kuhimiza wanariadha wa humu nchini kushiriki mazoezi katika hali mbalimbali za hewa,” akatanguliza Kipruto.

“Mbio za London Marathon ilitupa jukwaa zuri la kujifunza mengi, kwamba mambo hayawezi kuwa unavyotarajia yawe kila siku. Vyema kwa sasa kwa AK kubuni mikakati ya kuwaweka wanariadha wa Kenya katika hali ya kukabiliana vilivyo na hali mbalimbali za mabadiliko ya hewa – kwenye jua kali, upepo mkali, baridi, mvua, matope, nk.”

“Nilishindwa sana kuelewa jinsi Waethiopia wanavyomudu kufanya mazoezi katika mazingira ya baridi, mvua na upepo mkali. Kwa kawaida, huwa tunawapiku kirahisi sana iwapo hali ya hewa ni shwari,” akaongeza.

Matokeo yaliyosajiliwa na Kipruto katika London Marathon yalikuwa bora zaidi kuliko yale ya Boston Marathon ambapo aliambulia nafasi ya 10 mnamo Septemba mwaka huu.

“Nimekuwa nikitathmini matokeo yangu ya msimu huu baada ya kushiriki London Marathon. Sasa nalenga kupumzika vya kutosha baada ya kupona kabla ya kuamua na makocha wangu kuhusu mbio nitakazoshiriki mwaka ujao,” akasema Kipruto.