Michezo

Kipruto azima Kipchoge na kuvunja rekodi mbio za Tokyo Marathon

March 3rd, 2024 2 min read

NA GEOFFREY ANENE

BENSON Kipruto amelambisha sakafu Eliud Kipchoge akitawala mbio za Tokyo Marathon nchini Japan, Jumapili, Machi 3, 2024.

Katika raundi hiyo ya kwanza ya Marathon Kuu Duniani (WMM), bingwa wa Boston Marathon 2021 na Chicago Marathon 2022 Kipruto alikata utepe wa kwanza baada ya kukamilisha umbali huo wa kilomita 42 kwa saa 2:02:16. Muda wake bora katika 42km ulikuwa 2:04:02 kutoka Chicago Marathon 2023 kwa hivyo ameuimarisha kwa dakika moja na sekunde 46.

Mbali na kupata muda wake bora mpya, Kipruto, 32, pia alifuta rekodi ya Tokyo Marathon ya 2:02:40 ambayo Kipchoge aliweka mwaka 2022 akishinda makala ya 2021.

Alifuatwa kwa karibu na Wakenya Timothy Kiplagat (2:02:55) na Vincent Ngetich (2:04:18) walioimarisha muda wao kutoka 2:03:50 na 2:03:13, mtawalia.

Kipchoge, ambaye anashikilia muda bora dunia kwa watimkaji walio hai wa saa 2:01:09 baada ya mshikilizi wa rekodi ya dunia Kelvin Kiptum (2:00:35) kufariki Februari 11, 2024 alitarajiwa kufanya vyema.

Hata hivyo, mtimkaji huyo mwenye umri wa miaka 39, ambaye ni bingwa mara mbili wa Olimpiki na ameshinda WMM mara tano, aliambulia nafasi ya 10 kwa saa 2:06:50.

Kipchoge yuko katika timu ya taifa itakayoshiriki Michezo ya Olimpiki mwezi Julai/Agosti jijini Paris nchini Ufaransa. Ni marathon ya pili Kipchoge hajashinda kutoka 19 ameshiriki aanze mashindano ya 42km mwaka 2013.

Kenya ikisherehekea kurejesha taji la wanaume la Tokyo Marathon ambalo Muethiopia Deso Gelmisa alinyakua mwaka 2023, ilipoteza katika kitengo cha wanawake baada ya bingwa wa 2023 Rosemary Wanjiru kuridhika na nafasi ya pili kwa 2:16:14.

Wanjiru, ambaye aliimarisha muda wake bora kwa sekunde 14, alikamilisha katikati ya Waethiopia Sutume Kebede (2:15:55) na Amane Beriso (2:16:58), mtawalia. Mholanzi Sifan Hassan aliyekuwa amepigiwa upatu kuibuka malkia alikamata nafasi ya nne.

Matokeo ya Tokyo Marathon 2024:

Wanaume:

Benson Kipruto (Kenya) saa 2:02:16

Timothy Kiplagat (Kenya) 2:02:55

Vincent Ngetich (Kenya) 2:04:18

Hailemaryam Kiros (Ethiopia) 2:05:43

Tsegaye Getachew (Ethiopia) 2:06:25

Bethwel Kibet (Kenya) 2:06:26

Haimro Alame (Israel) 2:06:27

Simon Kariuki (Kenya) 2:06:29

Yusuke Nishiyama (Japan) 2:06:31

Eliud Kipchoge (Kenya) 2:06:50

 

 

Wanawake:

Sutume Kebede (Ethiopia) 2:15:55

Rosemary Wanjiru (Kenya) 2:16:14

Amane Beriso (Ethiopia) 2:16:58

Sifan Hassan (Uholanzi) 2:18:05

Betsy Saina (Amerika) 2:19:17

Hitomi Niiya (Japan) 2:21:50

Meseret Abebayahau (Ethiopia) 2:23:08

Khishigsaikhan Galbadrakh (Mongolia) 2:26:32