Habari Mseto

Kipruto Kirwa ataka serikali itangaze nzige janga la kitaifa

January 31st, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

MWANASIASA Kipruto Arap Kirwa ameisihi serikali kutangaza uvamizi wa ngige waharibifu kwenye mimea kama janga la kitaifa.

Bw Kirwa ambaye amewahi kuhudumu kama Waziri wa Kilimo chini ya utawala wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki mnamo Alhamisi alionya kuwa wadudu hao huenda wakasababisha baa la njaa, “ikiwa serikali haitaimarisha vita kudhibiti usambaaji wao”.

“Serikali itangaze wadudu hao kama janga la kitaifa ili suluhu kuwaangamiza ipatikane haraka iwezekanavyo, la sivyo mashamba yatasalia mahame,” akatahadharisha.

Kufikia sasa zaidi ya kaunti 10 zimetangazwa kuathirika na nzige, ikiwamo; Mandera, Wajir, Marsabit, Garissa, Meru, Isiolo, Samburu, Laikipia, Baringo na Kitui. Mapema wiki hii walionekana katika kaunti ya Makueni na ile ya Machakos.

Wadudu hao wanapotua kwenye shamba au eneo lenye mimea wanasababisha uharibifu mkubwa, jambo linalozua taharuki nchini.

Kulingana na Kirwa, serikali kupitia asasi husika, wizara na idara ya kilimo, ilipaswa kujua chanzo cha wadudu hao ili kuwazuia kusambaa zaidi.

“Tahadhari ilipotolewa, walipaswa kujua kiini hasa cha nzige hao (wanakotoka) wadhibitiwe kusambaa. Iwapo wangefanya hivyo, hatungekuwa tunazungumza kuhusu hasara ya mimea na mazao tuliyoshuhudiwa,” akasema mbunge huyo wa zamani wa eneobunge la Cherangany.

Wizara ya kilimo, serikali za kaunti zilizotajwa kuathirika na asasi husika, kwa ushirikiano zinajaribu kuangazia kero la wadudu hao.

Aidha, kuna maeneo wanayotumia ndege kupulizia dawa kuwaangamiza. Kwa mujibu wa maelezo ya waziri wa kilimo Peter Munya, shughuli hiyo inafanywa asubuhi na mapema kabla nzige hawajaanza kupaa angani, wakitafuta lishe.