Michezo

Kiptum, Akuta mabingwa wa mbio za nyika za MMTC

Na CECIL ODONGO August 5th, 2024 2 min read

WANARIADHA Abraham Kiptum na Christine Akuta ndio washindi wa mbio za kilomita 10 za Taasisi ya Kimatibabu na Teknolojia ya Mwale (MMTC) zilizoandaliwa mnamo Jumamosi, Agosti 3, 2024 Kaunti ya Kakamega.

Kiptum kutoka Kapsabet alishinda mbio hizo kwa upande wa wanaume baada ya kutimka kwa muda wa dakika 28:38 huku naye Akuta kutoka Eldoret akichomoka kwa dakika 33:51 kwa upande wa akina dada.

Kiptum aliwapiku Titus Rotich kutoka Iten aliyetumia dakika 29:04 naye Fredrick Domong’ole kutoka Pokot Magharibi akiibuka nafasi ya tatu kwa muda wa dakika 29:36.

Akuta alifuatwa na Maurine Chepkoech wa Iten kwa muda wa 34:07 huku Sharon Jemeli akiridhika na nafasi ya tatu baada ya kutumia  dakika 36:28 kwenye mbio hizo.

Kwenye mbio za kilomita nane, kwa wanaume Simon Maywa (Pokot Magharibi), Evans Kemboi (Mlima Elgon) na Linus Kembo walimaliza kwa muda wa dakika 22:57, 23:22 na 23:40 mtawalia.

Wanawake nao walishuhudia ushindani mkali kwenye mbio za kilomita sita, Dorcas Chepkemoi (Mlima Elgon) akimaliza wa kwanza kwa dakika 19:49 akifuatwa na Lonah Cherono (Kapenguria) dakika 20:32 na Veronica Chebet (Mlima Elgon) kwa dakika 20:46

Jonathan Akulima na Anita Morgan wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Shibanga (Mumias Mashariki) na ile ya Upili ya  Sitikho (Bungoma) mtawalia nao waliibuka washindi katika mbio za kilomita tano.

Akulima alitumia dakika 16:42 akifuatwa na Aaron (Shiraka sekondari) dakika 17:05:98 huku naye Russell Namakhanwa pia wa Shibanga akitimka kwa dakika 17:05:98

Morgan naye alitumia dakika 21:21 akifutwa na Michelle Buhdi wa Sitikho 21:22 na Esther Mwando wa Shule ya Upili ya Buluwe akitumia dakika 21:54.

Mbio hizo za Jumamosi zilijiri baada ya MMTC kuandaa matembezi ya kusaidia mwili kiafya mnamo Aprili mwaka huu, 2024. Pia mbio za marathon Makala ya kwanza ya MMTC yaliandaliwa mnamo Disemba 2023.

Mbio hizo zimekuwa zikiandaliwa kusaidia familia maskini kumudu gharama ya afya.

Mwanzilishi wa MMTC Julius Mwale alisema kuwa familia 5,000 ambazo hazijiwezi zitalipiwa ada ya kila mwaka ya Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF) na wadhamini.

Katika mashindano ya wikendi zaidi ya wanariadha 40 walishiriki ambapo walituzwa medali na pesa taslimu. Zaidi ya shule 10 ikiwemo zile za sekondari za Inaya, Imbale, Eluche, Shibinga, Shiraha, Buchenya, Shibanga, Bululwe, Bukolwe na Imanga zilizishiriki mbio hizo.

Wadhamini wa mbio hizo walikuwa ni INUA AI, Wazipay, Bit Media Africa, Hospitali za Hamptons na Optica. Wengine walikuwa ni Athletics Kenya, Shirika la Msalaba Mwekendu, Wakfu wa Tindi Mwale, ADAK, Mwal-Mart, Shule ya Kimatibabu kwenye Chuo Kikuu cha Maseno na Chuo Kikuu cha Masinde Muliro (MMUST).