Habari Mseto

Kiptum alikuwa ameanza mipango ya kutujengea jumba la kifahari, mkewe asimulia

February 13th, 2024 2 min read

CAROLINE WAFULA NA JOHN ASHIHUNDU

HUKU risala za rambi rambi zikiendelea kumiminika kufuatia kifo cha Bingwa wa Dunia Kelvin Kiptum na kocha wake, Gervais Hakizimana, mjane wake Asenath Jeruto amemtaja kama mume aliyekuwa na maono makubwa kwa familia yao.

Asenath amesema Kiptum alikuwa katika harakati za kujengea familia yao makazi ya kifahari katika eneo la Hillside mjini Eldoret, ambako wanariadha wengi wenye uwezo wanaishi.

Mjane huyo alisema mumewe alikuwa akisubiri kwa hamu ramani ya mjengo huo iidhinishwe na Serikali ya Kaunti ya Uasin Gishu ili ujenzi uanze na jumba likamilike kufikia Juni.

Asenath alikuwa akieleza jinsi mumewe alipenda jamii yake, huku akiongeza kwamba alikuwa mtu aliyejali zaidi maisha ya familia yake.

“Tulikuwa na mipango mizuri kwa maisha yetu ya baadaye. Hata alikuwa amepanga tuandamane hadi Uholanzi alikopangiwa kushiriki mbio za Rotterdam Marathon mnamo April 14 mwaka huu,” Asenath aliambia Taifa Leo huku akikumbuka mara ya mwisho walipokuwa pamoja mapema Jumamosi alipoondoka saa kumi alfajiri kwenda mazoezini katika kambi ya Flouspar akitarajiwa kurejea nyumbani Jumatatu.

Tulimuaga na kumtakia kila la heri kwenye mazoezi yake. Alitupigia baadaye mwendo wa saa nne akatuambia alikuwa amechoka kutokana na mazoezi.

Alitarajiwa kupeleka familia yake nje Jumapili kuburudika, lakini haikuwezekana kwa sababu alilalamika kuwa na maumivu ya kichwa baada ya mazoezi makali, mjane alisema huku akieleza jinsi walivyowasiliana kwa siku mara kwa mara hadi saa mbili usiku Jumapili.

Walikuwa wamezungumza kufikia saa kumi jioni, na alikuwa ameeleza kwamba alikuwa akielekea mazoezini pamoja na kocha wake, na baadaye akazungmza na watoto mwendo wa saa mbili usiku, akiahidi kuletea saa za mkononi Jumatatu, walipouliza awanunulie bidhaa hiyo.

Alikuwa ameahidi kumpigia wakati wa mapumziko wa mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kati ya Manchester United na Aston Villa lakini mjane akaamua kulala, kabla ya baadaye kuamshwa na mama mkwe mwendo wa saa tano usiku akimweleza kuhusu gari la mumewe kuonekana kando ya msitu wa Kaptagat.

Mwanzo, family ilikuwa imepata habari kwamba alikuwa ametekwa nyara, na kwa haraka walikusanyika na kuelekea mahali hapo, kabla ya kupata habari kwamba mwili wake umepelekwa Racecourse Hospital baada ya kuaga dunia katika ajali mbaya iliyotokea eneo la Kaptagat, kwenye barabaran kuu ya Eldoret-Eldama Ravine.

Bingwa huyo wa rekodi ya Dunia alikuwa akiendesha gari lake aina ya Toyota Premio ambalo lilipoteza mwelekeo na kutumbukia mtaroni kabla ya kugonga mti na kusimama mita 60 kutoka kwenye barabara hiyo.

Alipenda mazoezi na alikuwa na matumiani makubwa ya kutwaa ubingwa wa Rotterdam Marathon pamoja na taji la Olimpiki nchini Ufaransa.