Michezo

Kiptum aponea kifo alipogongwa na gari akishiriki Medellin Half Marathon

September 17th, 2018 1 min read

Na Geoffrey Anene

BINGWA wa mbio za Hannover Marathon mwaka 2012 Joseph Kiprono Kiptum ameponea kifo chupuchupu baada ya kugongwa na gari akiwania taji la Medellin Half Marathon nchini Colombia usiku wa kuamkia Jumatatu.

Tovuti ya Le Point imeripoti kwamba mkimbiaji huyu mwenye umri wa miaka 31, ambaye alikuwa anatafuta taji lake la pili mjini Medellin baada ya kushinda makala ya mwaka 2015, aliumizwa kidogo katika ajali hiyo.

“Mwanariadha huyu Mkenya, ambaye alikuwa anaongoza mbio wakati wa ajali hiyo, aligongwa na gari baada ya kuvunja sheria ya kutoingia katika sehemu magari yalikuwa yanapita,” tovuti hiyo imesema na kuongeza kwamba alisafirishwa hadi hospitali ya Medellin akiuguza majeraha madogo, ingawa yuko katika hali “nzuri”.

Katika mbio hizo za Medellin, mkimbiaji Juan Camilo Arboleda aliaga dunia kutokana na mshtuko wa moyo baada tu ya kukamilisha mbio hizi za kilomita 21. Mkenya Daniel Muindi aliibuka mshindi kwa saa 1:03:45.