Kiptum azoa Sh13m baada ya kushinda Valencia Marathon

Kiptum azoa Sh13m baada ya kushinda Valencia Marathon

NA GEOFFREY ANENE

MKENYA Kelvin Kiptum alitangaza ujio wake katika mbio za kilomita 42 kwa kishindo kikuu baada ya kutawala kivumbi cha Valencia Marathon Trinidad Alfonso kwa saa 2:01:53 nchini Uhispania, jana Jumapili.

Muda huo ni wa nne-bora katika historia ya mbio za 42km baada ya rekodi ya dunia 2:01:09 inayoshikiliwa na bingwa mara mbili wa Olimpiki Eliud Kipchoge aliyevunja rekodi yake ya dunia 2:01:39 mjini Berlin, Ujerumani mwezi Septemba mwaka huu.

Muethiopia Kenenisa Bekele alitimka 2:01:40 na kushinda Berlin Marathon 2019.

Kiptum alifuatwa kwa karibu na Mtanzania Gabriel Geay (2:03:00), Mkenya Alexander Mutiso (2:03:29), bingwa wa dunia Tamirat Tola kutoka Ethiopia (2:03:40) na mzawa wa Kenya raia wa Uturuki, Kaan Kigen Ozbilen (2:04:36).

Waethiopia Amane Beriso na Letesenbet Gidey walifagia nafasi mbili za kwanza upande wa akina dada.

Beriso alinyakua taji kwa 2:14:58. Alikosa rekodi ya dunia ya 2:14:04 inayoshikiliwa na Mkenya Brigid Kosgei kutokana na ushindi wake wa Chicago Marathon mwaka 2019.

Gidey anayeshikilia rekodi za dunia katika mbio za mita 5,000 na 10,000m pamoja na nusu-marathon alikamata nafasi ya pili kwa 2:16:51, ambao ni kasi bora kwa mwanadada anayeshiriki marathon kwa mara ya kwanza kabisa.

Wakenya Sheila Chepkirui na Fancy Chemutai waliridhika na nafasi ya tatu na tano mtawalia.

Chepkirui alikamilisha mwendo wa 42km kwa 2:17:29 naye Chemutai akaandikisha muda wa saa 2:18:11.

Kiptum na Beriso watazawadiwa Sh9.5 milioni kila mmoja kwa kumaliza katika vitengo vyao kwa chini ya saa 2:04:30 na 2:20:00 mtawalia.

Wataongezwa Sh3.8m kila mmoja kwa kuweka rekodi mpya za Valencia Marathon.

Wakenya Evans Chebet na Peres Jepchirchir walishikilia rekodi za Valencia Marathon Trinidad Alfonso kwa saa 2:03:00 na 2:17:16 mtawalia.

  • Tags

You can share this post!

Brazil wala njama ya kufinya Korea Kusini

WANTO WARUI: Serikali iweke mipango madhubuti ya masomo ya...

T L