Michezo

Kiptum na Kipserem wajishindia mamilioni Adnoc Abu Dhabi Marathon

December 8th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

WAKENYA Marius Kipserem na Abraham Kiptum wamejishindia Sh10,239,000 na Sh2,560,250 mtawalia baada ya kukamilisha makala ya kwanza ya mbio za kilomita 42 za Adnoc Abu Dhabi Marathon katika nafasi mbili za kwanza mnamo Desemba 7, 2018.

Kipserem na mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 21 Kiptum walikuwa bega kwa bega kwa kipindi kirefu kabla ya Kipserem kuongeza kasi katika hatua za mwisho na kukata utepe kwa saa 2:04:04.

Kiptum, ambaye rekodi yake ya Half Marathon ni dakika 58:18, aliridhika katika nafasi ya pili kwa saa 2:04:16. Wakenya hawa waliimarisha muda yao bora. Bingwa mara mbili wa Rotterdam Marathon nchini Uholanzi Kipserem alikuwa na muda wake bora wa saa 2:06:04 alioweka akishinda mjini Rotterdam mwaka 2017.

Inamaanisha kwamba ameimarisha muda wake bora kwa dakika mbili. Muda bora wa Kiptum katika mbio za kilomita 42 ulikuwa 2:05:26 aliotimka akimaliza Amsterdam Marathon katika nafasi ya tatu nchini Uholanzi mwaka 2017. Muethiopia Dejene Debela alifunga tatu-bora mjini Abu Dhabi kwa saa 2:07:06. Alijizolea Sh1,536,150.

Nafasi tatu za kwanza katika kitengo cha wanawake zilichukuliwa na Muethiopia Ababel Yeshaneh (saa 2:20:16), Mbahraini Eunice Chumba (2:20:54) na Gelete Burka kutoka Ethiopia (2:24:07). Mkenya wa kwanza katika kitengo hiki ni Caroline Kilel aliyefunga mduara wa tano-bora (2:29:14).

Mataji ya kitengo cha mbio za kilomita 10 yalinyakuliwa na Mkenya Richard Kimunyan (dakika 28:21) na Muethiopia Abeba Semanew (32:40).

Mwezi Septemba mwaka 2018, Rais wa Kamati ya Olimpiki ya Kenya (NOCK) Paul Tergat alihusika pakubwa katika uchoraji wa barabara zilizotumika kwa makala haya ya kwanza.