Dondoo

Kipusa alilia kuolewa na pasta

January 6th, 2020 1 min read

Na JOHN MUSYOKI

OTHAYA, NYERI

KIPUSA alishangaza waumini kanisani alipodai kwamba alifunuliwa ndotoni kuwa pasta ndiye atakayemuoa.

Inasemekana pasta wa kanisa hilo hakuwa ameoa na amekuwa akiambia waumini waungane naye kwa maombi ili Mungu amjalie mke mwema.

Siku ya kioja, demu mshirika wa kanisa hilo aliomba nafasi ya kutoa ushuhuda kuhusu jinsi Mungu alivyomtendea.

“Hamjambo? Leo nina ujumbe maalum kwa pasta wetu. Nimekuwa nikiota kwa takribani mwezi mzima tukifunga ndoa pamoja,” demu alianza.

Matamshi yake yaliwasisimua waumini, kila mmoja akaelekeza macho yote kwake, huku wengine wakiachwa vinywa wazi.

Watu wakaanza kunong’onezana katika ibada.

Demu akaendelea: “Nimekuwa nikiwaza na kuwazua, na mara nyingi huwa sipati hata lepe la usingizi. Mapenzi yangu kwa pasta yamenizidi.”

Muda si muda mwanadada alishindwa kuzuia hisia zake na kuanza kulia, huku akimwita pasta mpenzi wake.

Waumini wanaume walipigwa na butwaa na kubaki wameduwaa.

Hii ni kwa sababu inadaiwa kipusa huyo alikuwa amewakataa wengi wao walipomrushia mistari.

Kwa mtazamo wa makalameni hao, demu hakuwa na tamaa ya wanaume kama vipusa wengine mtaani.

Ibada ilisimama kwa muda ili kumtuliza kidosho, ambaye tayari alikuwa akiangua kilio kanisani akidai mapenzi yake kwa mtumishi wa Mungu yalikuwa ya dhati.

“Pasta, mpenzi wangu usiniache, wala usinivunje moyo. Ni mimi wako, na Mungu amenionyesha kwa ndoto,” demu akaendelea kulia.

Lakini pasta hakumfariji wala kutaka kumsikiza.

“Itabidi tuombe sana kwa sababu shetani hutumia mbinu mbalimbali kujaribu watu wake. Mungu pia atanifunulia nani nitakayeoa na sio mtu kujipendekeza tu,” mchungaji akasema.

Demu alishindwa kustahimili jibu la pasta, akaondoka moja kwa moja huku akidondokwa na machozi.