Dondoo

Kipusa atambua vya sponsa vina masharti

February 8th, 2019 1 min read

NA LEAH MAKENA

Kileleshwa, Nairobi

MWANADADA aliyekuwa akiishi kwenye nyumba moja ya kifahari mtaani hapa alilazimika kuhamia ushago baada ya kutemwa na sponsa kwa kujaribu kuwa na mpenzi wa kando.

Kidosho alikuwa na maisha ya starehe kwa zaidi ya miaka miwili aliponunuliwa nyumba ya kifahari, gari la kisasa na kumiliki biashara ya kufana aliyofadhiliwa na sponsa wake.

Mambo yalikuwa shwari hadi mwaka jana mrembo alipojaribu kuweka kijana wa rika lake kama mpenzi wake bila kujua kuwa alikuwa akihatarisha maisha yake ya raha.

Inasemekana kuwa mrembo alianza kuhisi upweke sponsa akiwa majuu na ndipo akaanza mapenzi ya siri na barobaro wa hapa mtaani.

Penyenye zasema kuwa sponsa aligundua mchezo wa kidosho kufuatia video aliyorekodi kupitia kamera ya siri aliyoweka nyumbani kwa mwanadada na akaamua kumpa funzo.

Siku ya kisanga, buda alifika nyumbani bila kumuarifu kipusa na kutaka kuchukua nguo zake na kuondoka. Kidosho hakuweza kujitetea. Aliitishwa funguo za gari, nyumba na duka badala ya kupatiwa nafasi ya kuzungumza.

“Unawezaje kuleta takataka kwa nyumba yangu ilhali ninakulisha na kukunywesha? Ondoka ukalishwe na hohe hahe unayedai kuwa mpenzi kwani nimemaliza shughuli yangu na wewe”, sponsa alichemka.

Juhudi za mrembo za kutafuta rafiki wa kumpa makao angaa kwa muda wa siku moja hazikuzaa matunda kwani wengi walimruka wakisema alikuwa akijigamba baada ya kuangukia sponsa.

Mrembo alilazimika kukodisha teksi na kufululiza hadi ushago shingo upande baada ya kukosa namna na haikujulikana iwapo alirejea mjini au la.