Dondoo

Kipusa atwanga polo aliyemhepa

December 15th, 2019 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

SANTONS, KASARANI

JOMBI aliyeishi katika mtaa huu alitamani ardhi ipasuke na kummeza mzimamzima, alipovamiwa na mrembo ambaye alikuwa amemhepa.

Duru zinasema mrembo alimvamia jombi na kumnyang’anya vitu vyake vyote vya nyumba kama adhabu ya kumtoroka.

Kulingana na mdokezi, wawili hao walikuwa wapenzi na mwanadada akamtaka polo wahalalishe penzi lao kwa kuoana.

Kumbe polo hakutaka uhusiano wowote wa kudumu na kidosho huyo.

Penyenye zinasema kalameni alianza kutafuta njia za kumhepa kidosho kisirisiri. Mpango wake ulitimia alipoamua kuhamia ploti nyingine ambayo mrembo hakuifahamu.

Waliomjua jamaa walisema amekuwa na mazoea ya kuhama ploti moja hadi nyingine, kwa sababu ya kuhepa vipusa.

Habari zilizotufikia zinasema baada ya kipusa kugundua kwamba jamaa alihama bila kumuarifu, mwanadada alikasirika sana na kuamua kumtafuta ili kumpa funzo kali.

Baada ya siku kadhaa walikutana naye. “Ulikuwa unafikiria sitakupata?” alimfokea jamaa.

Jamaa alishtuka sana kumuona kidosho. “Uliamua kunitoroka baada ya kunitumia kwa muda huo wote. Leo utanijua,” kidosho aliapa.

Taarifa zinasema kidosho aliingia chumbani mwa polo na kuanza kupanga vitu.

“Hakuna kitu nitakuachia hapa ndani. Umenipotezea muda wangu, leo hii ningekuwa kwangu,” kipusa alimkaripia kalameni.

Inasemekana mwanadada alimuita mtu wa mkokoteni baada ya kufunganya bidhaa hizo za nyumbani.

“Huyu jamaa kazi yake ni kuwatumia wasichana na kuwatoroka. Amehamia hapa kunihepa mimi,” demu aliwaambia wapangaji kwenye ploti.

Polo aliaibika sana lakini hakuwa na la kufanya ila kujichomoza ndani ya nyumba yake na kujificha.

“Mimi namjua. Hakuna siku utamuona bila msichana. Hata mimi aliwahi kunitongoza nikamkanya,” kipusa mmoja plotini humo aliongezea.

Kidosho alipanga kila kitu kwenye mkokoteni na kuondoka. “Ukitaka kuhama tena hama sasa,” mwanadada alimfokea jamaa huku akienda.