Dondoo

Kipusa awaka kupata sketi kitandani

July 31st, 2019 1 min read

Na LEAH MAKENA

SABAKI, SYOKIMAU

Mgogoro ulizuka katika nyumba moja eneo hili kipusa aliyemtembelea mpenzi wake alipowaka kwa hasira baada yakupata sketi ya mwanamke kwenye kitanda.

Mrembo alikuwa na mazoea ya kufika kwa mpenzi bila kumwarifu aliposhuku alikuwa na warembo wengi.

Siku moja kabla ya kidosho kufika, jamaa alikuwa amealika kikundi cha vijana wa kanisa lao kwake ili kuandaa mlo kwa ajili ya hafla waliyokuwa nayo kwa sababu nyumba yake ina nafasi ya kutosha.

Baada ya shughuli hiyo kukamilika usiku wa manane, polo aliwapa nafasi za kulala ili waraukie shughuli keshoye. Kwa heshima, jamaa alikubali warembo kujimwaga kwenye kitanda chake huku waume wakijilaza sakafuni na kwenye kochi.

Katika harakati za kuondoka mmoja wa warembo hao alisahau vazi lake kitandani na likazua zogo kidosho alipolipata saa saba mchana jamaa alipokuwa akihudhuria ibada.

Kwa machungu, kidosho alianza kutumia mpenzi jumbe za kushtua akimtaja kuwa kahaba aliyezoea kubadilisha wanawake kama nguo.

“Siku yako ya arobaini imefika leo, nimekuwa nikikushuku ila leo shetani amekuanika. Baada ya kurambishwa asali ulisahau kukumbusha mpita njia kubeba nguo zote?” kidosho alikejeli.

Jamaa alilazimika kuacha ibada ili kufika kusuluhisha mzozo huo ila akashindwa kidosho alipokosa kuelewa kuwa alikuwa na wageni usiku wa kuamkia siku hiyo.

Juhudi za polo za kuita majirani wamshawishi mpenzi wake ziligonga mwamba kwani alishikilia kuwa alikuwa akichezewa shere.

Kipusa aliondoka kwa dharau baada ya kurushia jamaa funguo sakafuni na kumtaka aendelee kualika warembo na kumtaka jamaa amsahau maishani.