Michezo

Kipusa kumzalia Aguero watoto ila kwa masharti

May 6th, 2019 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIPUSA Martina ‘Tini’ Stoessel ambaye kwa sasa anatoka kimapenzi na mwanasoka Sergio Aguero, amefunguka na kukiri kwamba atakuwa radhi kujipa kabisa kwa sogora huyo kiasi cha kumzalia watoto iwapo tu atakatiza mawasiliano yote na vichuna wake wa zamani.

Mbali na warembo Taylor Ward na Zoe Cristofoli, kichuna mwingine ambaye amewasha upya mwenge wa mapenzi yake na Aguero ni Karina Tejeda.

Karina aliwahi kumtoroka Aguero siku chache baada yake (Aguero) kuhusika katika ajali ya barabarani iliyomwacha na maumivu ya kuvunjika kwa mbavu jijini Amsterdam, Uholanzi mnamo Septemba 2017.

Ndoa kati ya Aguero na Tini ambaye ni mwanamuziki maarufu mzaliwa wa Argentina, ilianza kutokota mwezi jana baada ya Aguero kujumuishwa katika mojawapo ya video zilizofyatuliwa na kipusa huyo katika muziki wake.

Kubwa zaidi lililowafanya wawili hao kuwapa mashabiki wao kitu kipya cha kufuatilia, ni hatua ya familia ya Tini, ikiongozwa na mamaye Mariana, kuhamia jijini Manchester anakoishi kipusa huyo pamoja na Aguero.

Kwa muda sasa, Mariana amekuwa akisaidiana na mwanawe wa kiume, Fran kupakia mitandaoni picha za Tini zikiambatana na za Aguero ambaye kwa sasa huvalia jezi za Manchester City.

Mapema mwezi jana, Aguero alidhihirisha ukomavu wa penzi lake kwa Tini baada ya kuonekana wakibusiana peupe katika hafla ya kuadhimisha miaka 22 ya kuzaliwa kwa mrembo huyo.

Aguero ambaye bado ni tegemeo kubwa katika kikosi cha Argentina, aliwahi kufunga pingu za maisha na binti wa Diego Maradona, Gianinna na wakajaliwa mtoto wa kiume kwa jina Benjamin kabla ya ndoa hiyo kusambaratika mnamo 2012.

Nyota huyo anaanza kumtambalia Tini miezi michache tu baada ya kutemana na mrembo Taylor, 21 aliyehusiana naye kisiri. Taylor ni mwanawe mwanasoka Ashley Ward, 48, aliyewahi kuvalia jezi za Crewe Alexandra na Barnsley nchini Uingereza.

Kabla ya kupata hifadhi ya penzi lake moyoni mwa Aguero, Taylor aliwahi pia kumfungulia mzinga wake mwigizaji Sam Reece, 26, kabla ya tunda lake kuanza kudokolewa na beki matata wa Everton, Mason Holgate, 22.

Baada ya kuzidiwa na baridi ya upweke tangu atemwe na kichuna Karina mwaka jana, Aguero alianza kuburudishwa na mwanamitindo mzawa wa Italia, Zoe aliyewahi pia kutoka kimapenzi na kidume Andrea Ceroli na mwanahabari Fabrizio Corona.

Ceroli ni mshindi wa zamani wa shindano la Big Brother. Zoe alianza kumfungulia Aguero buyu lake la asali mnamo Oktoba 2018, mwezi mmoja baada ya mvamizi huyo kuhusika katika ajali ya barabarani jijini Amsterdam, Uholanzi.

Aguero mwenye umri wa miaka 30, alilimenya tunda la Karina, 32, kwa miaka minne kabla ya kutemana. Karina ana mtoto mmoja, Sol aliyepatikana katika uhusiano wa awali na dume jingine.