Dondoo

Kipusa taabani kuuza mali apate hela za mganga

November 19th, 2018 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

Kapolok, Teso

KIPUSA aliyekuwa ameolewa na polo mmoja wa eneo hili alitolewa kijasho alipotakiwa kuelezea sababu zilizomfanya kwenda kwa mganga kila wakati.

Inasemekana kipusa alishindwa kujieleza kwani maswali yaliyoibuliwa na ndugu za mumewe yalionekana kuwa magumu kwake.

Kulingana na mdokezi, makalameni walikasirishwa zaidi walipogundua kwamba kipusa alikuwa akiuza mali ya ndugu yao kisiri ili kupata hela za kumpa mganga.

Penyenye zinasema licha ya kipusa kufanya hivi kwa siri mumewe aligundua na kuwaarifu ndugu zake. ? “Hebu tuambie, unatafuta nini kwa mganga? Una njama gani kwa ndugu yetu,” makalameni walimuuliza kipusa. ? Kipusa aliamua kukaa kimya.

“Tumekuchunguza kwa muda mrefu. Juma halipiti kama hujaenda kwa mganga. Na huyo mganga tunamjua. Watafuta nini huko?” makalameni walimuuliza. ? Kipusa aliwaeleza kwamba alikuwa akienda huko kutafuta maombi.

“Huyo si mganga. Ni muombaji na huwa anakinga watu dhidi ya kukumbwa na majanga,” kipusa alieleza alipobanwa na maswali. ? Makalameni hawakutaka kusikia maelezo ya kipusa.

“Eti si mganga lakini anakinga watu dhidi ya kupatwa na matatizo. Huyo ni muombaji sampuli gani! Isitoshe huyo mtu unayedai tunamjua vizuri sana,” makalameni walishangaa.

Inadaiwa makalameni hao walimpa kipusa dakika tano atoe maelezo ya kuridhisha la sivyo wamtimue.

“Hapa kwetu umeona nani anahitaji maombi? Sema haraka,” makalameni walimshurutisha kipusa.

Kulingana na mdokezi, kipusa alikuwa akiuza mali ya polo apate nauli ya kwenda kwa mganga na pesa za kumlipa mganga huyo. ? Inadaiwa alipokosa jibu mwafaka, aliamua kuomba msamaha.

“Hatutaki msamaha wako. Ulipokuja hapa mali ilikuwa nyingi. Ndugu wetu hata jogoo peke yake hana. Umepelekea mganga,” makalameni walimkaripia kipusa.