Dondoo

Kipusa taabani kwa kutajataja 'ex' wake

May 6th, 2019 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

MATAYOS, BUSIA

Jamaa mmoja wa hapa alimuonya vikali mpenzi wake kwa kumlinganisha na mchumba wake wa zamani. Inasemekana polo hakufurahishwa na tabia ya mwanadada na akatisha kumuadhibu.

Inadaiwa kwamba mara kwa mara mrembo alikuwa akimlinganisha polo na mpenzi wake wa zamani.

Penyenye zinasema kukitokea mgogoro wowote baina yao, mwanadada alikuwa akitisha kurudi kwao na kisha arudiane na ‘ex’ wake.

“Umenifika kooni. Ukitaka kwenda kwa hicho kinyangarika chako wewe nenda,” polo alimkaripia kipusa. Jamaa alianza kumkemea kipusa huku akimrushia cheche za matusi.

“Una ujinga sana. Siku nyingine ukirudia tena kumtaja huyo mtu mbele yangu, walahi utajua kilichomnyoa kanga manyoya,” polo aliapa. Inadaiwa kipusa alilazimika kukaa kimya.

“Kama unajua hunipendi heri unieleze kuliko kila wakati kunilinganisha na huyo mtu,” polo alifoka.

Inasemekana watu wa familia walilazimika kuingilia kati. Walijaribu kusuluhisha mgogoro huo lakini jamaa alikaa ngumu.

Alisisitiza mwanadada alikuwa akimkosea kwa kumfananisha na mpenzi wake wa zamani. “Kama simtoshelezi heri aniondokee kuliko kushinda akiniambia jinsi ‘ex’ wake alivyokuwa mzuri kwake kunishinda,” polo alisema.

Inadaiwa majirani walicheka tu. Kipusa alipojaribu kupinga madai hayo, polo alimkemea huku akijaribu kumuadhibu.

“Ni mara ngapi nimeingia hapa na ukaanza kunitusi huku ukinilinganisha na mtu mwingine.

“Hata haikosi hii mimba umebeba ni yake,” polo alimfokea kipusa. Alisema kwa kumtaja mpenzi wa zamani kipusa alionyesha hakuwa akimpenda bali moyo wake ulikuwa kwa huyo licha ya kumuacha miaka mitatu iliyopita.

Watu wa familia waliamua kuacha jamaa akabiliane na hali yake. Kulingana na mdokezi, kipusa alilazimika kuomba msamaha huku akiapa kutorudia makosa yake.