Michezo

Kipute cha Kahi Indimuli chavutia zaidi ya vikosi 100

September 18th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

TAKRIBAN vikosi 120 kutoka eneobunge la Sabatia, Kaunti ya Vihiga vimethibitisha kushiriki kivumbi cha kuwania taji la Kahi Indimuli Raw Talent Search kitakachokunjua jamvi katika Shule ya Upili ya Chavakali mnamo Septemba 20, 2020.

Vikosi hivyo kutoka wadi saba tofauti za eneo pana la Sabatia vitashindana kuanzia kiwango cha mashindani kabisa kwenye mchujo utakaoshuhudia washiriki wakipunguzwa hadi 28 pekee katika hatua ya makundi.

Jumla ya vikosi saba vitatiwa kwenye makundi manne tofauti na washindi wawili wa kwanza kutoka kila kundi watafuzu kwa hatua ya robo-fainali.

Akihojiwa na mojawapo ya magazeti ya humu nchini, Maxwell Okwiri ambaye ni mratibu wa mashindano hayo alisema kwamba michezo hiyo pia itawapa washiriki na mashabiki fursa ya kuhamasishwa kuhusu madhila ya dawa za kulevya na umuhimu wa kuzingatia kanuni za kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19.

“Kaunti ya Vihiga imepata umaarufu katika ulingo wa soka baada ya kutoa mabingwa wa Ligi Kuu ya Soka ya Kenya – Vihiga Queens, Vihiga United na Vihiga Bullets ambao kwa sasa wananogesha Ligi ya Daraja la Kwanza,” akasema Okwiri katika mahojiano yake na Taifa Leo..

“Mapambano hayo yanadhaminiwa na Indimuli kwa lengo la kuwapa chipukizi fursa ya kutambua vipaji vyao na kujikuza kispoti,” akaongeza kwa kufichua kwamba washindi watatuzwa vinono.

 

Baadhi ya vikosi vinavyotazamiwa kunogesha mapambano hayo yatakayokamilika Novemba 2020 ni Red Devils, Vigogo United, Chavogere FC na Chandumba.