Kipute cha Kenya Cup charatibiwa upya  mchujo ukinukia

Kipute cha Kenya Cup charatibiwa upya mchujo ukinukia

Na CHRIS ADUNGO

KAMPENI za Ligi Kuu ya Raga (Kenya Cup) msimu huu sasa zitaanza rasmi mnamo Februari 27 wala si Februari 13 jinsi ilivyoratibiwa awali.

Hii ni baada ya vinara wa kamati ya ratiba ya mechi za ligi katika Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) kuafikiana na wenyeviti wa klabu zinazoshiriki kipute hicho kusogeza mbele tarehe ya kuanza kwa michuano ya Kenya Cup kwa wiki mbili zaidi. Hata hivyo, klabu za Mwamba RFC, Impala Saracens na Nondescripts zilitaka kivumbi hicho cha Ligi Kuu kianze Machi 6 ili kuwapa wanaraga wao fursa zaidi ya kujifua.

Mapendekezo yao yalifutiliwa mbali na KRU ambayo ilisisitiza kwamba kucheleweshwa zaidi kwa ligi kutaathiri maandalizi ya timu ya taifa ya wanaraga 15 kila upande, Kenya Simbas, inayotarajiwa kushiriki mapambano ya bara la Afrika kuwania taji la Gold Cup kuanzia Juni au Julai mwaka huu.

Mchujo wa kubaini vikosi viwili vya Ligi ya Daraja la Kwanza (Championship) vitakavyopandishwa ngazi kunogesha Kenya Cup msimu huu wa 2020-21 utafanyika wikendi hii.

Northern Suburbs watapepetana na wasomi wa USIU-A wikendi hii na mshindi atakutana na Strathmore Leos. Katika mchujo mwingine, Mean Machine ya Chuo Kikuu cha Nairobi itavaana na Egerton Wasps na mshindi atajikatia tiketi ya kukwaruzana na Chuo Kikuu cha Masinde Muliro (MMUST) RFC.

Mechi hizo za nne-bora zitatandazwa Januari 30 na washindi wawili wa mwisho ndio watapanda daraja kunogesha Kenya Cup kwa minajili ya kampeni za 2021 baada ya kujaza nafasi za Western Bulls na Kisumu RFC walioteremshwa ngazi muhula uliopita wa 2019-20.

“Tunasubiri kuona jinsi mechi hizo za mchujo zitakavyoendeshwa chini ya uzingativu wa kanuni zilizopo cha kudhibiti maambukizi ya Covid-19. Michuano hiyo itatuwezesha kubaini kiwango cha maandalizi yetu na iwapo zipo sehemu zaidi za kufanyiwa marekebisho ili kuwiana na kanuni za Wizara ya Afya na ile ya Michezo kabla ya Kenya Cup kuanza,” akasema mwenyekiti wa klabu za Kenya Cup, Xavier Makuba.

Kinyume na misimu ya awali, kampeni za Kenya Cup muhula huu zitashuhudia washiriki wakikumbatia mfumo tofauti wa wakipiga mechi za mkondo mmoja pekee.

Kwa mujibu wa mpangilio huo mpya, jumla ya mechi 11 pekee zikitandazwa kati ya Februari na Mei kabla ya nusu-fainali na fainali kutandazwa kwenye kipindi cha wikendi mbili zitakazofuata katika mwezi wa Juni.

Vikosi vya Kenya Cup havijawahi kushiriki mapambano yoyote tangu Machi ambapo kampeni zote za raga zilisitishwa kwa sababu ya janga la corona.

Wakati huo, Kabras RFC walikuwa kileleni mwa jedwali la Kenya Cup kwa alama 74, tatu zaidi kuliko wanabenki wa KCB ambao ni mabingwa watetezi. Homeboyz, Impala, Mwamba na Menengai Oilers walifuata.

Kwa mujibu wa KRU, wanaraga wa vikosi vya Kenya Cup watakuwa wakifanyiwa vipimo vya corona kila baada ya wiki mbili na mashabiki hawataruhusiwa kuhudhuria michuano hiyo uwanjani.

Vikosi vyote vilivyo na makao yao jijini Nairobi vilianza kufanyiwa vipimo vya corona uwanjani RFUEA hapo jana huku vile vya Nakuru na Kakamega vikitarajiwa kufuata mkondo baada ya wiki moja.

Kwa mujibu wa masharti ya Wizara ya Michezo, ni timu za taifa za Shujaa na Lionesses pekee ndizo ziliidhinishwa kuanza mazoezi kwa minajili ya Olimpiki zijazo za Tokyo, Japan.

  • Tags

You can share this post!

Ruto na Raila wazidi kuraruana kuhusu utawala wa Jubilee

BFK yafichua kikosi cha wachapanaji 15 watakaotegemewa na...