Michezo

Kipute cha voliboli ya walemavu kuanza Makueni

August 8th, 2018 1 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

Mashindano ya kitaifa ya voliboli ya walemavu yataanza Alhamisi na kumalizika Agosti 12 katika shule ya Makueni High School.

Kulingana na mwenyekiti wa Chama cha Voliboli ya Walemavu Nchini (KSVF), Polycarp Mboya, mashindano hayo yatatumiwa kuunda timu ya Kenya itakayowakilisha taifa katika mashindano ya kimataifa baadaye mwaka huu.

Mashindano ya kesho yatakayoanzishwa rasmi na Gavana wa Makueni, Kivutha Kibwana yatajumuisha wachezaji kutoka Kaunti zote nchini.

Wakati huo huo, Mboya ametoa wito kwa wahisani wajitokeze kusaidia timu kwa hali na mali kwa lengo la kuimarisha michezo miongoni mwa walemavu nchini.

Mboya alisema kwa siku za karibuni voliboli ya walemavu imepata umaarufu kote nchini, licha ya changamoto za ufadhili zinazotokea mara kwa mara.

Alisema ukosefu wa fedha ambao umekumba mchezo huo ndio uliosababisha Kenya kujiondoa katika mashindano ya bara Afrika yaliyofanyika mwezi Mei 15 na 22.

“Kote nchini tumeshuhudia uimarishaji wa voliboli ya walemavu katika viwango mbali mbali. Kila mahali nchini, timu zimeundwa katika viwango mbali, hasa baada ya Serikali ya Majimbo kuanzishwa,” alisema Mboya.

Alisema kufuatia shida walizopitia nchini Rwanda mashindano hayo yalipofanyika mwaka uliopita, kuna haja ya Serikali kuingilia na kusaidia kwa hali na mali.

Mboya alisema mashindano ya Makueni yatawapa nafasi wanamichezo wengi walemavu ambao baadaye wataiwakilisha nchi katika mashindano ya baadaye nchini na pia katika mataifa ya kigeni.