Makala

KIPWANI: Achanganya beats kunasa mashabiki

September 6th, 2019 2 min read

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

BAADA ya miaka mitano ya ku-rap, Beatrice Jeremiah Kimaro al-maarufu Mamalao amewashangaza mashabiki wake kwa kutoa kibao chake kipya Number 1 alichotumia mtindo mpya kabisa tofauti na alivyozoeleka.

Mamalao anasema anameamua kuchanganya beats kuvutia mashabiki zaidi.

“Nataka kujenga himaya kubwa zaidi yenye mashabiki wa mitindo tofauti hivyo sitajifunga na rapu peke yake,” akasema mwanamuziki huyu mkazi wa Mombasa.

Mamalao alijitosa kwenye fani ya muziki baada ya kushinikizwa na marafiki zake waliotambua kipaji chake mapema.

Yaonekana unawathamini marafiki zako sana

Mamalao: Naam! Wajua wanasema rafiki wa kweli ni rafiki wa siku zote iwe kwa dhiki au furaha. Wenzangu wamesimama nami kwa mengi hivyo waliponishinikiza nijitose ulingoni sikusita. Nilitumbukia mzimamzima na kuachia kibao changu cha kwanza Mdodo ambacho nimekitoa kwa lugha ya kinyumbani ya Ki-Taveta.

Ngoma zako zingine bado umeimba solo au una kolabo pia?

Mamalao: Niliwahi kushirikiana na Kidis na tukaachia Tusahau. Nimeimba pia na Fat S katika kibao Give Me Dat na Chikuzee katika Kipepeo. Lakini pia ninazo zingine nikiwa solo kama vile Ulikuwa Wapi na Sumu Kali.

Wasanii wa kike wamekuwa wakilalama kuhusu changamoto wanazopitia wanapotaka kurekodi ngoma au kutaka ichezwe na vyombo vya habari hasa maprodusa kushinikiza washiriki mapenzi nao. Wewe wakabilianaje na kikwazo hiki?

Mamalao: Ni kawaida lakini kila jambo hutegemea msimamo wa mtu binafsi. Ni muhimu sisi kina dada kuwa na msimamo thabiti na kukataa kutumiwa kama tambara mbovu. Ukiona produsa anahitaji mengine, achana naye. Maprodusa ni wengi na si wote wenye nia chafu.

Kibao chako kipya ‘Number 1’ kilitoka lini?

Mamalao: Agosti 23, 2019, na kinaendelea kufanya vyema hivyo kunipa mshawasha wa kuachia kazi zaidi kabla mwisho wa mwaka.

Unaazimia kufika wapi kimuziki?

Mamalao: Natamani sana kufikia kiwango cha STL wa Kenya anayeishi Norway na rapa Eve wa Amerika.

Una mipango ya kufanya shoo au kolabo nje ya nchi?

Mamalao: Kampuni nilionayo ya ATL Music imeanza mawasiliano na baadhi ya waimbaji wa Bongo kuhusu kufanya kolabo nao na endapo mipango itaingiana, midundo zaidi itatiririka.

Nini hasa kinaweza kuinua hali ya muziki hapa Pwani?

Mamalao: Tunahitajika kupendana na kuinuana kwani wasanii wengi huku kwetu wana vipaji lakini havitambuliki kwa kushindwa kurekodi nyimbo zao.

Unawashauri nini wanamuziki chipukizi?

Mamalao: Nawaambia wasikate tamaa kwani muziki una changamoto nyingi, ni juu yako kuwa na subira ili kuvuta heri na mwishowe utafanikiwa.

Unawaambia nini mashabiki wako?

Mamalao: Wasiwe na wasiwasi wowote kwani hata wao wamejionea niko ngangari kutokana na kibao changu kipya, kuna vingine kadhaa viko jikoni na havitachelewa kuiva.