KIPWANI: Akothee afungua roho

KIPWANI: Akothee afungua roho

NA SINDA MATIKO

MWANAMUZIKI mtatanishi na mjasiriamali kutokea Mombasa Akothe Okeyo amekuwa akitrendi sio kwa sababu ya muziki wake ila mahusiano yake mapya na mpenzi wake mzungu bwana Schwiezer almaarufu Omosh.

Hivi ulikutanaje na bwana Schweizer aka Omosh?

Ilikuwa 16 Julai 2022 kwenye ufuo wa Ziwa Zug kule Switzerland. Nilikuwa kwenye mkutano wa kibiashara uliokuwa umeandaliwa na rafiki yangu mmoja Pius. Kumbe Pius na Schweizer pia walikuwa ni washikaji. Tukiwa kwenye mazungumzo na kubadilishana namba, alichukua simu yangu na kusevu namba yake. Baadaye alinipigia na ndivyo tulivyoanza kuwasiliana.

Umekuwa kwenye mahusiano mengi mbona huyo kama vile kakutoa uchizi?

Kweli kanitoa uchizi ila ni kwa sababu ya vitu vingi. Mojawepo ni jinsi alivyosevu nambari yangu kwenye simu yangu. Aliandika Husband (Mume wangu). Sikujua hadi alipoomba nimpigie simu na niliposema sina namba zake za simu akaamua kupiga.

Enhee! Ila mapenzi yenu yamekuwa kwa kasi?

Sijui unataka nikueleze nini ila kiukweli kwa umri wangu huu, nimekuwa kwenye mahusiano kibao ila sijawahi kuwa na mwanamume aliyenifanya kuhisi mimi ni binti mdogo. Sahau kwamba nina watoto watano. Ni mwanamume anayenijali sana.

Kwa nini uliamua kuyaweka mahusiano yenu wazi?

Sababu yenu nyie wanahahabari. Mapaparazi hawakuniruhusu nipumue. Walikuwa wakinihusisha na kila mzungu na najua hii ni kutokana na mahusiano yangu ya awali.

Sikuwahi kutamani kuyaweka mahusiano yangu wazi ila hali hii ilinilazimisha sababu nilihusishwa kuwa kwenye mahusiano na mzungu yeyote ambaye alionekana kuwa karibu nami.

Unahisi wanahabari wamekukosea?

Ndio, sababu wameishi kunichorea picha ya kuwa mimi ni malaya. Ila siwahukumu baadhi yao wanatokea katika familia ambazo zimevunjika.

Aisee! Haya makubwa.

Baada yake kuonyesha nia, nilimshauri twende kwenye vipimo na hakusita. Baada ya vipimo vya HIV tulianza kudeti na ndani ya wiki tatu alikuwa amenitambulisha kwa familia yake.

Halafu kuna kipindi ulidai kuokoka?

Mwanzo kabisa sijui kama kunaye mtu asiyemhitaji Yesu Kristo katika maisha yake. Kingine, tasnia ya muziki wa kidunia imejaa machungu. Huna uhakika unayezungumza naye kama ni rafiki au adui. Wadau waliojaaa ni wauaji vipaji. Hujui kama unayemwona kuwa wa karibu wako kwenye gemu anakutakia mazuri au mabaya, hivyo hata kusukuma kazi zako inakuwa taabu. Ila kwenye injili mambo ni tofauti kidogo. Ndio sababu ya hatua ile.

Kwa uwezo wako wa kifedha umewahi kuwazia kuanzisha lebo?

Kamwe haiwezekani kabisa. Unajua ni kwa sababu gani? Wasanii wengi Kenya hawana heshima kabisa, ni wafitini, sio watu wa shukrani wamejaa majungu. Utamsaidia mtu kisha atakugeuka akupindishie maneno.

Ina maana hii ndio sababu ya wewe kufanya kolabo chache na wasanii wengi wa nyumbani?

Wapo wengi ambao wameniitisha kolabo. Lakini unapompa utaratibu fulani, kesho unaamka kusikia stori tofauti mara atadai ninamtongoza nataka nitoke naye na vitu vingi vya kipuzi. Watu hawajui tu mwenyewe nilivyohangaika kupata kolabo za kimataifa. Wakati mwingine hata nao hawasapoti kazi ambazo umefanya nao.

Bila shaka wewe ni mjasiriamali wa kupigiwa mfano, lakini pia umeweza kumudu kwenye muziki kwa muda mrefu. Umejifunza nini?

Kwamba sote hatuwezi kuwa wanamuziki. Halafu ili kufanikiwa kwenye muziki lazima upambane. Talanta pekee haitoshi. Asilimia 10 ni talanta na asilimia 90 iliyosalia ni kujituma na kutia bidii. Lakini zaidi kabisa, nidhamu yako ndio itakayoamua mafanikio yako.

Staili yako ya mavazi imezua kasheshe, hili unalizungumziaje?

Watu wasiumize akili, mimi sio kioo cha jamii ila ni kioo kwa wanangu. Ieleweke mimi ni mwanamke ninayejiheshimu, hata huko kwenye mavazi, navalia kulingana na tukio. Watu huwa wepesi kuhukumu pasi na kuelewa. Najielewa na najitambua sana na ndio sababu nimefanikiwa. Mengine sijali wa kusema na waseme watakavyo.

Kwa asiyekuelewa akakuchukulia kuwa mtu unayependa drama utamweleza nini?

Ndio mwenzenu napenda drama ndio hulka yangu. Lakini katika hilo napenda nidhamu sababu mwenyewe najiheshimu. Mimi ni mjasiriamali tena mwenye kisomo kizuri. Mimi ni mama, tena pia ni staa na sijali kama wanipenda au kunichukia. Kwa hiyo kila ninachokifanya ni kwa ajili ya wanangu sio watu wengine.

  • Tags

You can share this post!

Zukini na faida za kuila

Shabana FC kukabiliana na Mara Sugar kesho Jumamosi...

T L