Makala

KIPWANI: Hana choyo, kizuri anakula na chipukizi

March 22nd, 2019 2 min read

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

NI jambo la kawaida kwa wanadamu waliofanikiwa maishani kuvua nguo yao ya ungwana na kuvalia joho la ukatili na ubinafsi.

Ni wachache mno wanaoweza kudumisha ule utu na heshima kwa waja wenzao.

Na Elizabeth Nyambu maarufu Mama wa Rhumba kafanikiwa kwa hilo kwa kutumia lebo yake Royal Jek Entertainment iliyoko Mishomoroni, Mombasa kuwasaidia wasanii wanaoinukia angalao nao wapate mwangaza.

“Ni msanii niliyebarikiwa kuwa na studio yangu na sioni sababu ya kuwa na choyo kwa wanamuziki wenzangu ambao wanafika kwangu kwa ajili ya kuwarekodia nyimbo zao. Ni kawaida yangu kuhakikisha wote wanaorekodia hapa, wanafurahia kazi yangu,” asema Mama wa Rhumba.

Ni jambo gani hasa lilikufanya ujitose kwenye fani ya muziki?

Mama wa Rhumba: Muziki uko kwa damu yangu kwani wazazi wangu walikuwa ni wasanii wa ngoma za kitamaduni na hasa zile za Bumbumbu na Kayamba huko Mkomani, Kaunti ya Kilifi.

Ikiwa wazazi wako walikuwa wakiimba nyimbo za kitamaduni, mbona ukabadili mkondo?

Mama wa Rhumba: Tangu utotoni, nilikuwa napenda kuimba nyimbo nilizokuwa nazisikia kanisani na sikupenda ngoma za kienyeji wala sikuwahi kuzicheza hata mara moja.

Kibao chako cha kwanza kilipokelewa vipi?

Mama wa Rhumba: Wimbo wangu wa kwanza ulikuwa ni Usitatize Wanaosafiri ambao niliuzindua mwaka wa 2006 na kiuhakika ulitetemesha hewa hapa Pwani. Ndio wimbo ulionipa moyo wa kuendeleza kipaji changu.

Ilikuchukua muda wa miaka sita kuachia ngoma yako ya pili, mbona?

Mama wa Rhumba: Kibao cha pili Hawatakucheka Tena nilikiachia 2012 sababu nilitaka kukipa kile cha kwanza nafasi kuniundia jina na kupenya sehemu zote nchini na nchi jirani pia.

Je, uliwezaje kumiliki lebo yako hasa ikizingatiwa kuwa si kazi rahisi?

Mama wa Rhumba: Kwa hakika ni sababu ya kujinyima na kuweka akiba kutokana na mauzo ya kanda zangu na pia mshahara wangu sababu nilikuwa nimeajiriwa. Nilikuwa na nia ya kuhakikisha nimepata studio na baada ya miaka kadhaa, nilifanikiwa kwa hilo.

Je, umerekodi vibao vyako kwenye studio yako?

Mama wa Rhumba: Naam! Nilizindua wimbo wangu wa tatu wa Wakati wa Baraka Jumapili iliyopita kwenye studio hii na nina hakika utatamba kanda hii.

Wewe ndiye produsa pale ama umeajiri mtu?

Mama wa Rhumba: Ninao maprodusa mimi pia nikiwa mmoja wao na promota ambao tunashirikiana kuhakikisha tunaachia kazi nzuri.

Je, umeafiki ndoto yako katika ulingo huu wa burudani?

Mama wa Rhumba: Naweza sema ndio sababu tayari ninamiliki lebo yangu na pia ninawainua wanamuziki chipukizi ambao hawana uwezo wa kurekodi ngoma zao kwa kuwapa huduma hii kwa malipo ya chini.

Unawaambia nini mashabiki wako?

Mama wa Rhumba: Nawapenda sana na nawaomba waiunge mkono albamu yangu mpya ninayotarajia kuzindua karibuni kwani ina kila aina ya mitindo ya muziki ikiwemo Chakacha, Rhumba, Zouk na Zulu.

Tukimalizia, mbona wakakuita Mama Rhumba?

Mama wa Rhumba: Hahaha! Napenda kucheza Rhumba na hata ukisikiza ngoma zangu ingawa za injili, mtindo ni huo huo ndiposa mashabiki na wandani wakanibandika jina hilo.