KIPWANI: Hawa Nadra wan’leta ile vibe ya ‘Tatuu’

KIPWANI: Hawa Nadra wan’leta ile vibe ya ‘Tatuu’

NA SINDA MATIKO

MARA ya mwisho kwa tasnia yetu kuwahi kushuhudia kundi la muziki la kina dada ilikuwa ni katika miaka ya 2000.

Unakumbuka kundi la Tatuu, mabinti watatu waliotawala chati kweli kweli lakini miaka michache baadaye kundi likasambaratika.

Baadaye 2017 kukaibuka kundi lingine la mabinti wawili Band Becca na lingine la watatu Linda ambalo liliiteka chati za nchini na kutishia.

Band Becca kwa sasa wapo kimya.

Ila Linda wanaendelea kujitahidi kidogo lakini sasa wanafahamika kama Nadra, huku likiwa na wanachama wawili pekee Raych na Alexis.

Mlipotoka kama Linda, mlikuwa watatu Raych, Alexis na Beryl, sasa mumerudi mkiwa wawili tu?

Raych: Beryl aliamua kujitoa ili afanye mambo yake.

Vipi, kulizuka ugomvi kati yenu?

Raych: Wala hapakuwepo na tatizo kati yetu. Mwanzo kabisa wajua kundi la Linda nililianzisha mimi na Beryl kisha baadaye tukaja kukutana na Alexis na kumwongeza. Kuondoka kwake hatukutarajia, tulishangaa. Hakutupa sababu hivyo tukahisi kuwa huenda alikuwa na majukumu mengine yaliyohitaji muda wake zaidi ya kuwa na kundi.

Mlikutana vipi?

Raych: Mimi na Beryl tulikutana 2014. Promota na mwanamuzki Wawesh Mjanja (mumiliki wa Penya Records & Uwezo Org) alikuwa ameitisha usahili wa waimbaji, tukashiriki na kupasi. Miaka miwili baadaye akajiunga nasi Alexis na Wawesh akapendekeza tuunde kundi na ndipo ikazaliwa Linda Januari 2017.

Kufanya kazi chini ya Wawesh ilikuwaje?

Alexis: Mwaka wa kwanza mambo yalikuwa mazuri sana. Hatukua na mkataba ila baada ya sisi kutia saini mwaka uliofuatia, mambo yakabadilika. Wawesh akageuka na kuwa mhuni katika usimamuzi wa kazi zetu, tukawa hatumwelewi.

Ndio chanzo cha Linda kufa?

Alexis: Ndio sababu alipotupa mkataba tulisumbuana sana sababu mambo mengi hayakuwa yamekaa sawa. Ulikuwa ni mkataba wa unyanyasaji. Kila tulipomuuliza mbona hapa hapajakaa sawa, akawa anatufokea. Tulisumbuana kwa muda lakini baada ya miezi kadhaa tukafikia mapatano na ndipo tukasaini. Hata hivyo, mambo hayakutunyookea. Alianza kutulaghai sana. Dili tulikuwa tunapata kibao ila akawa anatulaghai kwenye malipo. Kwa mfano tungepata dili la Sh300,000 angetuambia kwamba ni laki sababu waliokuwa wakitusaka walipitia kwake. Baadaye tukaja kugundua na kila tulipomuuliza, akawa mjeuri sana kwetu. Hapo ndipo tukafikia uamuzi wa kujitoa. Tulivunja mkataba ule na kuachana naye kisha tukaamua kuanza kundi jipya baada ya kukaa kimya kwa muda tukijipanga.

Kundi lenyewe ndio Nadra sasa?

Alexis: Ndio. Wakati tunaunda kundi hili, tayari Beryl alikuwa amejitoa. Nafikiri pia usumbufu wa Wawesh ulimfanya kukata tamaa. Tuliamua kubadili jina ili kuja kivingine kabisa, tayari tumeshaachia EP yetu ya kwanza Love teaser.

Linda sasa Nadra, mbona majina ya Kiswahili?

Raych: Sababu sisi Waswahili bwana. Linda tulikuwa watatu na tulijitahidi sana kulinda kundi na muziki wetu. Sasa ni Nadra tukiwa na upungufu wa mwanachama mmoja lakini pia muziki wetu sio wa kawaida, una upekee, ni muziki nadra.

Sio makundi mengi yametoboa kudumu kwa muda mrefu, mnaona mkifanikiwa?

Raych: Hii ni ishu ambayo tunaiwazia kila siku. Lengo letu ni kudumu kwa kipindi kirefu kama Sauti Sol na tunaamini tunaweza sababu tunaelewana sana mapungufu na uwezo wa kila mmoja wetu. Tunaheshimiana lakini kubwa zaidi tunachungana sana kuhakikisha kuwa mmoja wetu hatelezi.

Kwa miaka ambayo mmedumu kwenye gemu, mna yepi ya kusema kuhusu tasnia yetu ya muziki?

Alexis: Wanamuziki wa kike tunakabiliwa na changamoto kibao na ndio sababu sio wengi wetu wanaofanikiwa kudumu. Tasnia imejaa wahuni. Wasanii wa kike sisi huchukuliwa kama chombo cha ngono. Huwezi kupewa fursa kwa sababu ya uwezo wako. Wengi wanaojifanya kuwa wenye koneksheni kwenye gemu, mara nyingi hututaka kingono ili watusaidia au watupe nafasi. Ni moja kati ya changamoto ngumu tunayopambana nayo.

  • Tags

You can share this post!

Starehe Boys kufadhili elimu ya mvulana mwerevu baada ya...

KASHESHE: Amber Lulu apata sapoti

T L