Makala

KIPWANI: 'Hiki kimya si bure, narudi kwa vishindo'

May 24th, 2019 2 min read

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

WASANII wengi iwe ni mwanamuziki, mchoraji au mwigizaji huwa na sababu maalumu za kuwa na jina la utani au ukipenda la kubandikwa, wengi wao wakijipa ama kupewa kutokana na umaarufu wa yale wanayotekeleza kwenye sanaa wanazohusika nazo.

Na hilo si tofauti kwa Abdulrahman Ahmed Khalifa kutoka Lamu ambaye alibandikwa jina la ‘Mfalme wa Visiwani’ na mashabiki wa muziki wa eneo hilo ingawa anajulikana kote Pwani na sehemu nyingine za nchi kwa jina la Dully Da Brown.

Hii ni kutokana na mtindo wa ngoma zake ambazo ni mchanganyiko wa Bongo na Bajun Flava.

Dully ameathiri nyoyo za wapenda muziki wa visiwa vya Bajuni vikiwemo vile vya Rasini, Tchundwa, Mbwajumwali, Pate, Kizingitini, Kiunga, Ndau na Nyabogi kati ya vinginevyo kutokana na kuimba nyimbo zenye lafudhi na mahadhi ya Kibajuni.

Nini kilikufanya ujitose kwenye fani ya muziki ?

Dully: Nilijiingiza katika fani hii ya muziki kutokana na mamangu kuwa mtunzi mzuri wa mashairi. Nilitamani kuwa mwimbaji ili nipate kutumia baadhi ya mashairi yake kwenye nyimbo zangu.

Na je, umeweza kutunga nyimbo ukitumia mashairi ya mama?

Dully: Naam! Ngoma kama vile Wananichukia na Uchekechee Nkono.

Wimbo wako wa kwanza ulikuwa upi, uliuzindua lini na uliitikiwa vipi?

Dully: Kibao changu cha kwanza kiliwa Please Binti, nilikizindua 2007 na kiliitikiwa vizuri hasa na wakazi wa sehemu zote za Lamu ambao walinipa moyo kwa kunialika kwenye tamasha mbalimbali.

Kuna msemo ‘ambacha ukucha’ ambao unatumika sana sehemu ya Lamu na kuna wimbo wako wenye maneno hayo, kautunga wewe ama uliazima tu?

Dully: Huu msemo ulikuwapo hapo awali lakini nilipouimba ulizidi kkuwa maarufu zaidi sio huku kwetu tu bali hata kwengineko nchini na hata Zanzibar na Tanzania.

Hebu tupashe nyimbo zako nyingine ambazo zimepata umaarufu na ni mitindo gani hasa unayotumia?

Dully: Ngoma kama vile Masifa, Napagawa, Uchekechee Nkono, Nibusu na Sikuachi. Nachanganyachanganya mitindo kama vile Mduara, Bongo Flava na mahadhi ya nyimbo za kikwetu pia.

Umefanya kolabo au ni basi, wewe tosha?

Dully: Ndio nimeshirikiana na Sudi Boy na Kidis the Jembe kwenye nyimbo za Ambacha Ukucha na Nisamehe.

Je, waweza kusema kuwa vyombo vya habari vimekukuza?

Dully: Ndio kwa kiasi kikubwa sababu ngomza zangu zachezwa kwenye stesheni mbalimbali za Pwani, KBC, na Citizen. Pia kule TZ natamba kwenye Maisha Magic Bongo.

Una jambo gani kuhusu muziki na wanamuziki wa Pwani?

Dully: Kiuhakika muziki uko hali ya juu na kuna wanamuziki wazuri sawa na wale wanaosifika hapa nchini na nchi jirani. Lakini tatizo wanamuziki hatupendani na wale ambao wana uwezo wa kutusaidia, hujitia hamnazo. Ningewaomba viongozi wetu watuunge mkono na kutusaidia badala ya kuwanufaisha wasanii kutoka nje.

Unawaambia nini mashabiki wa muziki wako?

Dully: Nawaomba wazidi kuwa na subra kwani subira huvuta heri. Hiki kimya changu si cha bure, najifunza mengi kwa hii sanaa na nikirudi, nawaahidi narudi kwa vishindo!