Makala

KIPWANI: Hupata nyimbo katika ndoto na zikawa hiti

November 8th, 2019 2 min read

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

AMEBAHATIKA mara tatu kujiwa na nyimbo akiwa usingizini na alipoamka, aliweza kuzihifadhi na kuhakikisha ameziimba.

Huyo ni msanii wa Mombasa, Jane Katiku ambaye angali anafurahia nyimbo zake hizo tatu, ‘Ole wako Mwanadamu’, ‘Jina la Yesu’ na ‘Hakuna wa Kufanana’.

“Mashairi ya nyimbo hizo tatu yalinijia usingizini na ndizo zilizonipa motisha wa kuweza kutunga nyimbo nyingine tano kukamilisha albumu yangu ya kwanza ya nyimbo nane ya Ole Wako Mwanadamu,” akasema Jane.

Msanii huyo anaamini kuwa wakati utafika atatambulika sababu ya mapenzi yake kwa Mungu.

“Sitakata tamaa bali nitafanya bidii zaidi kuhakikisha nimefika pale ninapoazimia na kwa uwezo wake Bwana, nitafanikiwa,” akasema msanii huyo mcheshi.

Ndoto hizo hasa zilikuwa na maana gani kwako?

Jane: Kwa hakika ndoto nilizoota za nyimbo hizo tatu, zilinifanya nitumbukie katika bahari ya kuhakikisha nimekuwa msanii wa kutambulika.

Nyimbo zako nyingine tano ni zipi?

Jane: Nyimbo zangu tano zilizoko kwenye albam yangu hiyo ya kwanza ya Ole Wako Mwanadamu ni Ngathima ya lugha ya Kikamba, Utukufu, Ilikupendeza, Nena Nami na Msifadhaike.

Ni kipindi gani umezindua albamu yako hiyo?

Jane: Niliizindua albamu yangu hiyo mnamo mwezi wa Mei mwaka huu na nashukuru inazidi kuitikiwa.

Una nia ya kufika wapi katika fani ya muziki?

Jane: Nataka niendeleze kipaji changu cha muziki nitambulike kimataifa.

Kwa nini umeamua kuwa mwimbaji wa nyimbo za kumsifu Mungu?

Jane: Niliinukia nikiwa nimeokoka na nilitaka kueneza Injili kwa njia ya uimbaji.

Umewahi kufanya shoo zozote Mombasa, Pwani ama sehemu nyingine za nchi?

Jane: Ndio nimewahi kualikwa kuimba katika makanisa mbalimbali ya hapa Mombasa na nina mpango wa kwenda sehemu nyingine za nchi mapema mwakani.

Ni changamoto zipi unazopata katika fani ya muziki?

Jane: Changamoto kubwa ni matapeli wanaorekodi kanda zangu na kuziuza. Sikupata kuungwa mkono na yoyote kunisaidia kunilipa gharama za kurekodi nyimbo zangu hizo ila ni kazi yangu ya kushona nguo mtaani Migadini ndiyo imenisaidia.

Ni wasanii gani wanaokukosha ambao unatamani kufanya kolabo nao?

Jane: Ninampenda sana Cristine Shusho na Martha Mwaipaja wa Tanzania na ningependa kufanya kolabu naye. Pia ninazipenda nyimbo zake Eunice Njeri wa hapa nchini, ninatamani niimbe naye.

Wasanii wanawake hulalamika wanasumbuliwa na maprodusa wanaotaka yao yasiyohusiana na muziki, wasemaje wewe?

Jane: Ni kawaida kwa mwanamke yoyote sio wasanii peke yao wanaotakikana na wanaume lakini kuna kukubali na kukataa. Nashukuru produsa wangu tunafanya biashara ya muziki na wala hakuna lingine kati yetu.

Unaazimia kutoa albamu nyingine lini?

Jane: Niko kwenye mipango ya kutayarisha albamu nyingine ninayotegemea kuizindua mapema mwaka ujao.

Umewahi kwenda nje ya nchi kwa ajili ya muziki?

Jane: Ndio nimewahi kufika Arusha nchini Tanzania ambako nilikwenda na kwaya ya kanisa kurekodi nyimbo za Injili katika Radio Maalum.

Una wako wa maisha?

Jane: Niko katika harakati za kumchagua wangu wa maisha ambaye nataka awe kama mimi mwenye kufuata nyendo zinazoambatana na mapenzi ya Mungu.

Unawaambia nini mashabiki wa nyimbo zako?

Jane: Nawaambia wazidi kusikiliza nyimbo zangu na wasubiri kwa hamu nyimbo zangu mpya ninazotarajia kuzizindua mwakani.

Unawashauri nini wanamuziki chipukizi?

Jane: Nawashauri wasife moyo katika uimbaji wao na wale wanaofikiria wana vipaji wajitose katika fani hii ya muziki, kesho ya mtu hujulikana na Mungu.