KIPWANI: Kaingiza zigo la mwisho sokoni

KIPWANI: Kaingiza zigo la mwisho sokoni

NA SINDA MATIKO

UKIKUTANA naye, kuna vitu viwili visivyoweza kuyakwepa macho yako. Staili yake ya kunyoa. Kanyoa upara na kuacha kichwa kiking’aa kama bati jipya la kuezekea nyumba.

Lakini kubwa hata zaidi ni hulka yake ya uchangamfu anayoinogesha kwa tabasamu ya mara kwa mara. Huwezi kuamini sifa hizi zimesitiri siri nzito za mtu aliyewahi kupambana na sonona na hata wakati mmoja kuwazia kujitoa uhai wake.

Huwezi kuamini magumu haya yalimkuta mwigizaji wa haiba ya Kevin Samuel mzaliwa na mlelewa wa Mombasa. Ndio, yule staa wa kile kipindi cha NTV, Mali.

Nilipokutana naye wiki tatu zilizopita, Kevin ambaye ni kakake mkubwa mtangazaji maarufu wa zamani wa TV Janet Mbugua, alikuwa mchangamfu ajabu.

Aisee! Kaka umechangamka sana, vipi umepandishwa cheo?

Hahaha! Acha masihara wewe. Ila Eeeh! Leo ni siku kubwa kwangu, siku spesheli. Ni uzinduzi rasmi wa series mpya Igiza ambayo nimehusika. Natumai mtaipenda.

Ina maana uzinduzi huu ni mkubwa zaidi ya kazi zote ulizozifanya?

Ndio! Sababu Igiza ndio kazi yangu ya mwisho kama mwigizaji. Nimeamua kustaafu nikajishughulishe na mambo mengine. Niliyoyafanya kwenye uigizaji naamini yametosha. Naamini historia itanikumbuka vyema.

Hujaigiza toka 2015, halafu leo umehusika kwenye mzigo mpya unasema ndio funga kazi?

Nilishafanya uamuzi huo zamani, sio wa leo. Niliposita kuigiza 2015, tayari uamuzi nilikuwa nimeufanya. Huku sikuwa narejea kwenye gemu, hapana! Wajua Mali kilikatizwa ghafla hivyo nilihisi sikuwa nimetimiza malengo. Nilihisi itakuwa vyema kama nikiaga kwa kushiriki kazi moja ya mwisho na kazi hiyo ikawa ni Igiza.

Mbona ilikuchukua muda kufanya hivyo?

Wajua siishi Kenya tena. Nikija nafanya kama kutembea tu. Nilibahatika kukutana na mke wangu kwenye mishemishe hizi za uigizaji. Na muda mfupi baadaye familia yangu ikahamia Paris, Ufaransa. Huko ndiko ninakoishi kwa sasa na isitoshe, nipo shuleni nikisomea masuala ya Afya ya Umma, pamoja na kozi za utoaji ushauri nasaha. Kwa sababu hizo siwezi kuendelea na uigizaji.

Kwa hiyo ulitokea Paris kuja kuigiza ‘Igiza’?

Hapana! Ilinikuta tu kwa bahati mbaya. Nilikuwa hapa nyumbani halafu ikatokea ile lockdown, hivyo singeweza kusafiri sababu kipindi hicho nilipaswa kuwa London. Ndipo nikapata mwaliko wa kushiriki Igiza. Nikaona badala ya kupoteza muda acha nijiweke bize na pia nilitaka kufanya kazi ya mwisho.

Kwa nini usingekataa sababu ulikuwa tayari umejitoa, au hela tamu?

Kusema ukweli wangu wa dhati, wala halikuwa suala la mpunga. Wajua nilipopewa uhusika wa Reggie, kusema kweli ulinigusa sana. Kama mtakavyokuja kuona, Reggie ni mtu aliyebarikiwa. Anaishi maisha ya kutamanisha, ila hana amani wala furaha kabisa, anahangaishwa na msongo wa mawazo na pia ndoa yake inayumba. Vitu hivi vinamsukuma kuwa mlevi chakari na mwishowe kuishia kumponza na kumharibia maisha kabisa. Kwa utathmini wa mbali, stori yake ilinigusa sana sababu na mimi kama nisingelikuwa makini, ningeishia kuwa kama yeye.

Kivipi?

Mwenyewe nilihangaishwa sana na uraibu wa pombe iliyosababishwa na mimi kuugua sonona. Niliporejea Kenya kwa muda mfupi 2019, moja kwa moja nilijipeleka Rehab na baada ya miezi minne nikawa sawa. Kwa maana hiyo kama nisingelijitahidi kuwa sawa, ningeishia kuwa kama Reggie.

Pia umewahi kukiri kutaka kujiua?

Hali hii ilitokana na msongo wa mawazo. Nilikuja kugundua nimekuwa nikitatizwa na sonona kwa muda mrefu sana na ni 2018 ndipo nilipata picha kamili. Kabla ya hapo tayari nilikuwa nishajaribu kujitoa uhai. Nakumbuka siku moja Julai 2007 nikitokea nyumbani Mombasa kuja Nairobi, niliabiri treni na wakati wa safari nikaamua ndio nitamaliza safari yangu duniani. Nilirusha mizigo nje ya dirisha. Nilitaka kujirusha ila sijui ni kipi kilichonizuia. Itakuwa ni watu sijui, itakuwa ni usalama kwenye treni sijui. Ila nakumbuka nilipofika Nairobi sikuwa na chochote. Nilipofika nilijaribu kutembea madukani nikisaka chochote chenye sumu ninywe nife. Niliishia kujikuta kwenye duka moja la kuuza vyuma na rangi na nilipoitizama ile mikebe, nikaamua acha kwanza nipigie simu familia yangu kuwaaga. Ile simu ndio iliniokoa sababu walinionyesha mapenzi mazito sana na kunishawishi vinginevyo.

Sasa hali vipi?

Nashukuru hayo yamepita sasa. Napata mafunzo ya kuwa mshauri nasaha, nataka kuwasaidia watu wengi zaidi wanaopitia hali ngumu za kiakili.

Ila wewe ni msomi sana, vitabu vimekukubali…

Haha! Nafikiri elimu ni kitu bora na ukipata fursa, jielimishe. Isitoshe, wazazi wetu walitusisitizia sana suala la elimu.

Sasa unasomea shauri nasaha na Afya ya Umma, hizi si nyongeza tu?

Eeh! Nimefanya kazi kama mwanafulusi. Nina uelewa mzuri wa uchumi na fulusi sababu nimewahi kuwa broka wa hisa, Stanbic. Sasa hivi naendesha biashara zangu na pia kuwasaidia watu kuanzisha biashara zao.

Kipi kingine umesomea?

Muziki. Nilijiunga na chuo cha muziki cha Berklee College kule Boston, Marekani 2002 kusomea shahada. Nilisita kidogo kabla ya kurejea na kumalizia 2008. Nilifunza somo la muziki katika shule ya sekondari ya Aga Khan Academy Mombasa, ndiko nilikopata masomo yangu ya sekondari.

Uigizaji nao ulikupataje?

Kwa bahati mbaya. Nilikuwa kwenye pati moja hivi halafu akaniambia mtu usaili wa kipindi cha Changes ulikuwa ukifanyika. Niliamua tu kujaribu na nikaishia kupata uhusika wa Kuta Sempele, mwanasheria msaidizi wa wakili Alfred Gitau.

Hivi ni kipi kingine tusichokijua?

Kwamba pia niliwahi kuwa jaji wa usaili wa shindano la Tusker Project Fame. Nilifahamika kama Judge Kevin na wengi hawakunipenda sababu sikupenda mzaha. Lakini pia kama hamjui, nimewahi kutunga nyimbo na kuwatumbuiza marais Daniel Moi na Mwai Kibaki kwenye hafla tofauti kule Mombasa. Watu wengine mashuhuri niliowahi kuwatumbuiza ni His Highness Aga Khan na Alicia Keys alipozuru Kenya.

 

Unajua wewe ni mwanamuziki usiyefahamika sheikh?

Hapo ndipo huwa mnakosea. Sihitaji kuwa na wafuasi milioni Instagram. Wakati mwingine unaweza kuwa mwanamuziki bila hata kuwa na mashabiki ila uwe na uelewa mzuri wa nini kinachotakiwa kuwa mwanamuziki.

Bwana acha nikuache tusije anza kubishana bure hapa?

Haha! Asante kwa muda wako.

  • Tags

You can share this post!

Wito kwa serikali ipunguze ushuru kwa pembejeo

DOMO: Walichomea picha shangazi Riri!

T L