Makala

KIPWANI: 'Kama si mama, singekuwa hapa'

August 16th, 2019 2 min read

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

HUWA ni rahisi mno kwa msanii chipukizi kupiga hatua za haraka endapo mlezi wake atampa sapoti.

Kwa Mohammed Rai al-maarufu Rich Junior, mamake ndiye shabiki mkuu na hilo limempa ari ya kuendeleza kipaji chake. “Mamangu alikuwa mwimbaji wa ngoma za kitamaduni huko Mariakani na ni yeye alinifanya nipende muziki na hata kunisisitizia nijitose katika fani ya muziki,” asema Rich Junior.

Ulianza muziki lini?

Rich Junior: Mwaka 2014 nikiwa darasa la saba nilipotunga wimbo wangu wa kwanza wa Yaliniumiza Mapenzi.Niliachia kibao hicho 2015 nikiwa darasa la nane na mama ndiye alinisaidia kukizindua.

Ukiwa darasa la nane bado umri mdogo, mbona ukaimba wimbo wa mapenzi?

Rich Junior: Kiuhakika nilichelewa kusoma, hivyo hapo nilipokuwa darasa la nane, nilikuwa na umri wa miaka 22. Mamangu alifurahi sana kuwa ndoto yake ya mimi kuwa mwanamuziki ilitimia japo haukuitikiwa vizuri.

Una nyimbo nyingine zozote ulizotoa baadaye?

Rich Junior: Naam! Sikati Tamaa, Maisha Yangu na Ahsante Mama na hizi mapokezi yalikuwa mazuri.

Una wanamuziki wanaokukosha ambao una hamu kuwa kama wao?

Rich Junior: Kwa hakika nawahusudu sana waimbaji wa Bongo kina Aslay, Ruby na Nandy na Otile Brown hapa nyumbani. Natamani nifikie viwango vyao.

Azma yako?

Rich Junior: Jibu langu ni sawa na la kila mwanamuziki la kufika kileleni na kutambulika kimataifa. Nataka nitambe hapa nchini kabla ya kutikisa kwa majirani.

Kuna wanaokupa sapoti mbali na mama yako?

Rich Junior: Hakika namshukuru sana Bernard Ondimu al-maarufu Ajiwa Stance. Japo ni msanii wa injili, Stance ananisaidia sana katika harakati za kurekodi kazi zangu.

Ukiwa msanii wa kizazi kipya, ni changamoto gani unazokumbana nazo?

Rich Junior: Kwa hakika, changamoto kubwa ni gharama za kurekodi nyimbo zetu. Suluhisho laweza kupatikana kama serikali za kaunti zitatusaidia kwa hilo.

Mambo gani unafikiria ukiwa nayo ama ukiyapata yanaweza kukusaidia kuinua kipaji chako?

Rich Junior: Kupiga shoo ndani na nje ya nchi. Kwa sasa napiga shoo kwenye sherehe za harusi na bethdei hapa Pwani na ninapoalikwa na wasanii wenzangu.

Una lipi la kuwaambia wapenzi wa nyimbo zako?

Rich Junior: Nawaomba wazidi kuniombea na kunipa sapoti nifanikiwe kuwapa mapya kila wakati.