KIPWANI: Katoi wa Tabaka alivyosalia na ‘baby face’

KIPWANI: Katoi wa Tabaka alivyosalia na ‘baby face’

NA SINDA MATIKO

WAPO watu waliojaliwa neema ya kusalia na nyuso za kitoto hata umri uwasonge vipi.

Mmoja wao ni Katoi wa Tabaka. Mara yangu ya kwanza kumcheki akipiga shoo ni wikendi iliyopita nilipokuwa zangu Pwani nilipokwenda kusaka mchuzi wa pweza ili unifanyie ile kitu.

Baada ya shoo pale Swahili Pot Hub, nikamfuata msela kumpongeza.

Bwana kaka ile shoo umeua ujue?

Asante sana ila. Ama acha tu.

Ila nini tena?

Mimi na bendi yangu tulikuwa tumejiandaa na nyimbo nyingi za kuwatumbuiza. Waandalizi walifanya kutuharakisha, hamkupata utamu wote. Itakuwa ni sababu mgeni mheshimiwa yule Balozi wa Ufaransa alikuwa na haraka kidogo? Sasa wa kulaumiwa sio Balozi ila waandalizi sababu tungeanza mapema kidogo. Ila hamna neno nimefurahia kuona wengi mlifurahia muda mchache tuliokuwa nao. Kuna siku nyingine tu.

Kweli kabisa. Naomba niulize jambo la kizushi, hivi kakangu una umri wa miaka mingapi?

Aah! Miaka tena? Kuna tatizo au?

Hapana ni ule ukomavu wa seti yako wewe na bendi nzima, kidogo imenigusa?

Aaah! Kwetu ni Malindi nimezaliwa 1983, hesabu nafikiri sasa unayo. Mimi ndio kitinda mimba kwenye familia ya watoto watatu.

Basi utakuwa na tabia za kupenda kudekezwa?

Kwa nini?

Sababu wewe kitinda mimba.

Ndio tatizo lenu nyie wa mjini. Maisha yangu hayakuwa ya hivyo. Wazazi wangu walikuwa wakulima na kawaida majukumu ya vitindamimba hasa watoto wa kiume kwenye jamii yetu ilikuwa ni kuchunga mbuzi kwenye bonde na vilima vya Marafa.

Acha wewe?

Eeeh! Na huko ndiko chimbuko la muziki wangu. Wajua tukiwa malishoni na vijana wenzangu, tulikuwa na muda mwingi, ili kupitisha muda tulikuwa tukitunga nyimbo za kila aina na hata kuwa wabunifu kwa kutengeneza ala za muziki feki feki ilimuradi zitoe milio itakayokwendana na nyimbo zetu za malishoni.

Ala kama zipi?

Kuna ala kama kaupinde hivi tulikuwa tunakaita Kadama, nyingine ya kupuliza tuliyoita Kipopoi na Milozi. Yalikuwa ni maisha matamu sana. Hayakuwa maisha ya presha na majukumu kama sasa.

Kweli malisho yalikuandaa.

Kipaji changu kwa wenzangu kilikuwa zaidi kwenye utunzi wa nyimbo wao wakiwa wazuri kwenye ala. Baadaye nilijiunga na kwaya ya kanisani kisha kwaya ya shule ya msingi na nikiwa shule ya upili nikajihusisha sana na klabu za muziki, uigizaji na sanaa.

Shule ya upili umejiunga mwaka gani?

1998, na huko nikakutana na kundi la muziki wa rapu TABAKA Rap Crew na nikawa mwanachama. Kwenye muziki hii ni familia yangu. Ngoma yetu ya kwanza tuliachia 1999 na ilifanya vizuri tu hapa nyumbani.

Ikawaje uliacha rapu na kuanza muziki wa asili?

Baada ya masomo yangu ya shule ya upili nilikwenda kusoma Ulaya. Nikiwa kule nikawa nahudhuria matamasha mbalimbali nikiwa na marafiki zangu kutoka Senegal na Ghana. Huko kujichanganya na wana hao kutoka Magharibi mwa Afrika ndio kulinifanya nianze kuupenda na kuuthamini muziki wa kitamaduni sababu wale wanapenda sana miziki ya asili yao.

Kwa hiyo ukaanza kutunga nyimbo za kiasili ukiwa kule?

Hapana. Baada yangu kurudi Kenya, nikajiunga na kundi la sanaa la Malindi ambapo muziki wa asili ulipewa kipaumbele sana. Na hiyo ikawa chimbuko la Mijikenda Jazz Band.

Safari ya Mijikenda Jazz Band imekuwaje?

Imekuwa nzuri, mafanikio yamekuwa kiasi cha haja. Tumeshiriki kwenye shoo kadhaa kama vile Safaricom Jazz, Koroga Festivals, Coco Festival kati ya zingine kibao.

Mna nyimbo ngapi?

Tuna albamu moja kwa sasa inayoitwa Kunani na ina nyimbo zaidi ya nane.

Kando na matamasha, mna kijiwe mnakotumbuiza mara kwa mara?

Kila Ijumaa tupo pale Tamu Beach Resort, Jumamosi utatukuta Mwembe Resort kisha Jumapili tupo pale Paparemo Beach Restaurant.

You can share this post!

CECIL ODONGO: Uhuru kama mwenyekiti azungumzie siasa na...

Asukumwa jela miaka 5 kwa kumrusha mwanadada kutoka orofa...

T L