Makala

KIPWANI: Kibao kwa mama kilimtosa ulingoni

September 13th, 2019 2 min read

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

WANASEMA penzi la mama tamu na ili kudhihirisha hilo, msanii Nelly Kendi al-maarufu Nezz Kenya alimtungia mamake kibao Malezi Yako Mama ila kwa bahati mbaya aliaga dunia kabla hakijazinduliwa.

Wingu la giza lilitanda maishani mwake lakini hakufa moyo. Alikizindua lakini alikifinya marekebisho kidogo.

Pole kwa msiba. Hebu tupashe zaidi kuhusu kibao hicho ulichomtungia mama.

Nezz: Nilikuwa nimeutayarisha wimbo huo mnamo Novemba, 2017 nikitarajia kumpa ‘surprise’ mamangu wakati wa sikukuu ya Krisimasi. Lakini kabla ya kukizindua mama akalazwa hospitalini na akafariki dunia Januari, 2018.

Pigo hilo halikukuathiri kiasi cha kutaka kuachana na muziki?

Nezz: La hasha! Mama alitaka niwe msanii na ingawa aliaga dunia, nilitaka kutimiza ndoto yake kwangu. Namshukuru baba na ndugu zangu kwa kunipa sapoti.

Umesema ulikifanyia kibao chako cha kwanza marekebisho. Fafanua

Nezz: Nilikibadilisha jina na kukiita Malezi Yake Mama na kukiachia Julai 2018 na kusema kweli ingawa ilikuwa ni audio, kilikubalika vyema.

Umeachia kazi zingine?

Nezz: Nimeandaa lakini si wajua changamoto kubwa kwetu chipukizi ni hela za kurekodi. Hivyo bado nasakanya wadhamini niweze kurekodi lakini pia nimejitosa katika uigizaji na huenda hilo pia limechangia kuchelewa kuvizindua.

Inamaanisha huimbi tena?

Nezz: Sijaacha muziki ila nilingilia uigizaji kwa sababu hauna gharama kubwa na unaweza kuachia haraka filamu fupi fupi ambazo zinavutia wapenzi wa fani hiyo.

Ulifanikiwaje kujitosa katika uigizaji ama una mdhamini?

Nezz: Nilianzisha kikundi changu cha Nyota Arts katika eneo la Likoni ambapo nilianza nikiwa na waigizaji wawili lakini hivi sasa tuko na wasanii 27.

Mmeachia filamu zozote?

Nezz: Ndio tumeshatoa filamu 12 za vichekesho na kuna filamu moja; The Spirit ambayo natarajia kuizindua mwishoni mwa wiki hii.

Unashikilia nafasi gani ugizaji?

Nezz: Mara nyingi hushiriki kama mhusika mkuu.

Unawezaje kusawazisha fani hizi mbili hasa ikizingatiwa kuwa zote zahitaji kujitolea pakubwa?

Nezz: Ni kibarua kigumu lakini bidii na nidhamu zimeniwezesha kuangazia yote mawili bila moja kuniponyoka.

Unapania kufika wapi katika fani hizi mbili?

Nezz: Nataka jina langu liwe kubwa sio tu hapa nyumbani bali Afrika nzima na ikiwezekana duniani kote. Maadamu nimetia nia hiyo, najua nitafanikiwa.

Wawaambia nini mashabiki wako wa muziki pamoja na uigizaji?

Nezz: Wasibanduke, mambo matamu yaja kwa mshindo. Aidha pia wanifuatilie Facebook kwa jina la Nezz Beibe Kenya na Instagram hivyo hivyo na YouTube Nezz Kenya.