Makala

KIPWANI: Lengo langu kusaidia maskini, si kujitanua

November 15th, 2019 2 min read

SHAWN Gabriel almaarufu Tyrell asema amejitosa kwenye fani ya usanii sio kujitajirisha bali afanikiwe kuwa msanii maarufu ili kipato atakachopata kisaidie wasiobahatika.

Tyrell anasema aliwaza na kuwazua kutafuta njia ya kuwasaidia watoto mayatima na machokoraa ambao hawakubahatika kuishi maisha sawa na wale wenye wazazi wao wanaopata malezi mazuri.

“Niligundua nitakapokuwa mwanamuziki wa kutajika na, maarufu, nitafanikiwa kupata kipato ambacho kingi ninadhamiria kisaidie nyumba za watoto mayatima na kutafuta mpango wa kuhakikisha wale wanaoishi barabarani, wapate sehemu watakazoishi maisha bora.

“Nilifikiria na kuamua nia yangu hiyo ya kusaidia nilipokuwa kidato cha pili na wazo langu hilo nililifanyia kazi mara nilipokamilisha masomo yangu ya Kidato cha Nne,” akasema Tyrell.

Ulikuwa na hakika gani utakuwa mwimbaji mwenye jina kubwa?

Tyrell: Niliamini kwa kuwa nilikuwa na nia nzuri tena ya kusaidia watoto waliopoteza wazazi wao, nilijua Mungu atanibariki kwa lengo langu hilo.

Tuambie ulianza safari yako hiyo lini na unaendeleaje?

Tyrell: Niliipangia safari ya mafanikio nikiwa Kidato cha Pili na nilianza kazi ya kwanza kwa kutoa kibao changu cha kwanza, Roseate Lights.

Je, wimbo wako huo uliitikiwaje?

Tyrell: Kibao changu hicho niliimba pamoja na wenzangu wawili Ceaser Qym na Tony, kiliitikiwa vizuri lakini wenzangu hao waliendelea na masomo ya juu na nikabakia peke yangu.

Ulifanyaje ukiwa peke yako?

Tyrell: Nilijifunza nikiwa na kampuni ya Eden Pix Media njia za kunifanya niwe produsa na nikafanikiwa kwa hilo.

Ulishikilia kazi ya uprodusa ama pia uliendelea na nia yako ya kuwa mwimbaji?

Tyrell: Nilifanya kazi ya uprodusa na pia nikaweza kutoa kibao changu cha pili, Tam Tam ambacho nilikizindua miezi miwili iliyopita. Mashallah, nyimbo hii iliitikiwa vizuri kiasi cha kufanya baadhi ya stesheni za redio kuniita kwa mahojiano.

Una wimbo wowote mwingine unaoazimia kuzindua?

Tyrell: Ndiyo. Wimbo wangu wa tatu ‘Let me go’ natarajia kuuzindua wakati wowote mwezi huu wa Novemba.

Unatumia mitindo gani kwa nyimbo zako na kwa sababu gani?

Tyrell: Nyimbo zangu natumia mtindo wa RnB sababu najua ndio unaopendwa zaidi na mashabiki wangu.

Unahisi utafanikisha lengo lako la kusaidia wasiojimudu wakiwemo mayatima?

Tyrell: Ndio, nina tamaa kubwa kwani nimeanza kuona dalili na hata nimeanza kuwasaidia baadhi ya watoto wanaorandaranda barabarani. Nataka niendeleze kipaji changu niweze kuinua hali yangu ya uchumi nizidi kutimiza lengo langu.

Una nia ya kufika wapi kimuziki?

Tyrell: Nina nia kubwa ya kuwa mwanamuziki wa kimataifa. Nikitambulika kote duniani, nitakuwa na kipato kikubwa ambacho zaidi ya nusu yake, nitakitumia kusaidia wasiojiweza.

Ni wanamuziki gani wanaokukosha?

Tyrell: Katika Afrika Mashariki, Diamond wa huko Bongo ndiye ninayemshabikia zaidi na Chris Brown wa Marekani ndiyr chaguo langu la mwanamuziki bora duniani.

Unawaambia nini mashabiki wa muziki wako?

Tyrell: Nawataka wazidi kuniunga mkono na mimi nawaahidi kuwa watapokea vibao moto moto kila baada ya mwezi mmoja ama miwili.

Wanazumiki munatambulika kuwa wenye kujitosa kwa mapenzi, wewe ukoje?

Tyrell: Kiuhakika kwa wakati huu sijiingizi katika mapenzi sababu najua nikijihusisha, nitashindwa kutimiza lengo langu. Lakini nitakapokuwa tayari kuwa na wangu wa maisha, nitaamua kuwa na huyo mmoja pekee.