Makala

KIPWANI: Lil Mizze ataka wasanii Pwani washirikiane kufanya eneo zima kitovu cha talanta

June 13th, 2020 2 min read

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

ANA imani kubwa atafika mbali kimuziki hasa kwa kuwa hivi sasa yuko chini ya menejimenti ya Dkt Giuseppe Moscarino anayeazimia kujenga jumba la orofa 61 hapo mjini Watamu ambalo litajulikana kwa jina la Palm Exotjca.

“Kwamba niko chini ya usimamizi wa Moscarino anayetarajia kujenga jumba kubwa zaidi barani Afrika hapa Watamu, nina matumaini makubwa nitapiga hatua kubwa ya kuinua kipaji cha uimbaji wangu kitambulike kote Afrika Mashariki,” amesema Philip Tuwei almaarufu Lil Mizze.

Mwimbaji huyo aliye pia mchezaji wa soka pamoja na soka ya ufukweni, anasema ujenzi wa jumba hilo utakapotimia, hautamsaidia yeye binafsi bali pia utasaidia kuinua sanaa ya muziki katika mwambao wa Pwani

“Sina shaka wala tashwishi kuwa wasanii wa hapa Pwani tutanufaika na matumaini yangu ni kuwa tutakwenda sambamba na waimbaji maarufu wa sehemu nyingine ya nchi pamoja na wale wa huko nchini Tanzania,” akasema Lil Mizze.

Kibao chake alichokitoa siku nyingi hazijapita ni kile cha ‘Toto’ ambacho anaamini kitaendelea kuitikiwa vizuri na anawataka mashabiki wa kazi zake za sanaa waingie YouTube na ku-subscribe ikiwa ni njia moja ya kumuunga mkono na kumpa moyo wa kuendelea kutoa nyimbo nyingine.

Msanii na mwanamichezo Philip Tuwei almaarufu Lil Mizze. Picha/ Abdulrahman Sheriff

Lil Mizze anasema ngoma hiyo ya ‘Toto’ ameimba pamoja na Reed Malis na kukirekodi kibao hicho katika studio ya Beast Mode Records.

Wimbo wa ‘The winning Rock Palm Exotjca’ aliimba pamoja na Titia Tola mjini Mombasa produsa akiwa P Baindo.

Msanii huyo wa Pwani amewahi kufanya shoo na Mejja wa The Kansoul huko mjini Eldoret katika Platform ya Mambo Mseto iliyoongozwa na B Mzazi, Willy M Tuva.

Nia yake kubwa ni kuhakikisha ameinua kipaji chake hadi kileleni anakolenga kila mwanamuziki anayejiamini kwani hapo ndipo atatambulika sio nchini Kenya pekee bali kote barani Afrika na dunia nzima.

Kwa waimbaji anakoshwa na kazi za wanamuziki kina Khaligraph Jones, Susumila, Kelechi, Africana, Naiboi, Redsan, Ethic Entertainment na wengineo.

Lil Mizze ana kikundi chake cha wasanii kinachoitwa Exotic Gang ambacho kina Sukaka Jatwo, Mike Hip Hop Kid na Young Millie.

Mwanamuziki huyo anaamini kama wasanii maarufu wa Pwani watajumuika na wale wanaoinukia, sehemu hiyo itakuwa na wanamuziki watakaotamba sawa ama zaidi ya wale ambao ni maarufu katika kanda hii ya Afrika Mashariki.

Lil Mizze anaamini wasanii wa Pwani wana vipaji na kama wale waliopata umaarufu watajumuika na kushirikiana na chipukizi, eneo hilo litakuwa kitovu cha wanamuziki wa kutambulika sio Afrika Mashariki pekee bali kote barani Afrika.

“Pwani lina waimbaji wenye vipaji na ambao wakipata motisha kutoka kwa wenzao wenye majina makubwa, wataweza kupanda ngazi na kuwa sawa na wale wanaotajika kwa wakati huu,” akasema Lil Mizze.

Msanii na mwanamichezo Philip Tuwei almaarufu Lil Mizze. Picha/ Abdulrahman Sheriff

Aliwahi kutoa albamu yake ya nyimbo saba kwa sauti na video ikiwa ni ya pili ambayo ina nyimbo za ‘Kameme’, ‘Shikilia’, ‘Presha’, ‘Kijicho’, ‘Expensive Nigga’, ‘Mshike’ na ‘Kutafuta’.

Nyimbo hizo amezirikodi katika studio za Big Foot Records Kongowea mjini Mombasa, produsa akiwa P Baindo; Wakawaka Records ya Watamu Posta, produsa Kimambo na Neptune Records ya Mtwapa, produsa Lameck Boy.

Mitindo ya nyimbo aliyotumia kwa albamu yake hiyo ni Kapuka style, Dancehall, Riddim na Hip Hop.

“Mashabiki wa muziki wa wakati huu, wanapenda mitindo ya kurusha roho ambayo ni ya kujirusha yakidijitali na ndiyo nimetumia kwa nyimbo zangu,” akasema Lil Mizze.

Mbali na albamu yake hiyo ya pili, Lil Mizze ametoa wimbo wa ‘Serebuka’ ambao amefanya kolabo na Paneli; wimbo ambao ameurekodi katika Studio ya Wakawaka Records, produsa akiwa Kimambo.