Makala

KIPWANI: Qasida yamsaidia kukwepa maovu

April 26th, 2019 2 min read

Na ADDULRAHMAN SHERIFF

PAMOJA na kutoka kwenye mazingira yenye kutambulika kuwa na ukosefu wa usalama na vijana wengi kuathirika kwa dawa za kulevya, kijana Abubakar Said ameweza kujiepusha na changamoto hizo kwa kujiingiza kwenye sanaa ya Qasida na Nasheed.

Said, almaarufu Abubakar Ramly akiwa kiongozi wa kikundi cha Fityatul Imaan, amefanikiwa kujiepusha na majanga yaliyoko sehemu anayoishi eneo la Kibokoni mjini Mombasa kwa kujumuika na wenzake wawili kutoa video za Qasida za kumsifu Mtume Muhammad.

Akiwa na Abubakar Said Mahmud na Hashim Zeinuddin, Ramly amepania kuhakikisha wanafikia viwango vya wasanii wa kimataifa kama kina Maher Zein, Sami Yusuf na wengineo ambao Qasida zao zinawika kote ulimwenguni.

Lipi lilokufanya ujitose kwenye fani ya Qasida?

Ramly: Nilijihusisha kwenye uimbaji wa Qasida ili nijiepushe na mambo ambayo yangeliathiri maisha yangu.

Albamu ya Qasida yako ya kwanza ilikuwa ipi, uliitoa lini na iliitikiwaje?

Ramly: Nilitoa album yangu ya kwanza mnamo Mei 2016 iliyokuwa ya Qasida nne, Quran, Mama, Usihuzunike na Karibu ya Ramadhan. Kwa YouTube, Qasida ya Mama ndiyo iliyosikilizwa na mashabiki wengi zaidi kwani hadi mwishoni mwa wiki iliyopita, ilikuwa tayari imesikilizwa mara 295,473.

Ni usia gani hasa ulitoa kwenye Qasida hiyo ya Mama hata ikavutia mashabiki wengi?

Ramly: Ni kumshukuru mama kwa kunizaa na pia kunivumilia kwa malezi na taabu nyingine zilizompata tangu nikiwa mchanga hadi kufika ukubwani.

Baada ya Qasida hizo nne, kuna nyingine zozote ulizotoa?

Ramly: Tuko nazo Qasida tatu nyingine ambazo ziko tayari, tunategemea kuzirekodi hivi karibuni. Hizo ni Yatima, Tuwaangalie wanawake kwa jicho la huruma na Tuisome elimu.

Kwenye kuimba kwako Qasida, huwa unatoa kwa mahadhi yako mwenyewe ama unaiga mahadhi ya waimbaji wengine?

Ramly: Qasida ya Mama tulitungiwa na kutiliwa mahadhi na Imam Nizar hali nyenginezo tunatunga na kuzitia mahadhi sisi wenyewe.

Kuna waimbaji ama vikundi vyovyote vya Qasida ambavyo vinakuvutia?

Ramly: Mimi ni shabiki wa mwimbaji wa Qasida, Brother Nassir na kikundi ambacho nakipenda ni kile cha Shirko Media.

Umewahi kualikwa kwenye hafla zozote kwenu Mombasa, nchini Kenya ama kwengineko nje ya nchi?

Ramly: Huwa mara nyingi naalikwa kwenye harusi na hafla za Madrassa. Nimewahi pia kualikwa Mombasa na huko Dar es Salaam nimewahi kupata ualishi kutoka kwa Hureira kwenye tafrija ya Baitul Halal.

Ni changamoto gani unazopitia katika safari yako ya kuinua kipaji cha uimbaji wako na kufikia malengo yako ya kuwa mwimbaji wa kimataifa?

Ramly: Tatizo kubwa ni ukosefu wa udhamini kwani ni karibu miezi kadhaa tumekamilisha Qasida zetu tatu lakini hatujazirekodi kwa ukosefu wa fedha.

Ni jambo gani ambalo ukilipata linaweza kukufanya ukapiga hatua kubwa na ya haraka ya kupata mafanikio?

Ramly: Nina uhakika nikipata mdhamini, mimi pamoja na wenzangu tutaweza kufanikiwa kwa haraka

Una mipango yoyote ya kusafiri kwenda ng’ambo kwa ajili ya kupata ujuzi zaidi wa kuimba Qasida?
Ramly: Ninatamani sana nipate safari ya kwenda kuonana na kina Maher Zein na Sami Yusuf kwani kuonana na waimbaji hao na kupata ushauri wao, kunaweza kunisaidia nikawa sawa na wao. Lakini tatizo ni lile lile la ukosefu wa fedha.

Unawaambia nini mashabiki wako?

Ramly: Nawaambia wanaopenda Qasida zangu kwamba hazitapita siku nyingi, watafurahi kwani kabla ya kuanza kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan, nitatoa Qasida ya Ramadhan ambayo inadhaminiwa na Al-Ihsan Foundation na nina hakika wataifurahia!