KIPWANI: Toto la Kitaita lateka anga ya uigizaji

KIPWANI: Toto la Kitaita lateka anga ya uigizaji

NA SINDA MATIKO

INAWEZEKANA umewahi kupitia kwenye kibanda chake ukajipatia kinywaji kitulizo ili kupunguza makali ya kiu kutokana na jua la Mombasa.

Au ulikuwa umejilaza kwenye kochi ikarushwa Telenovela ya Pete kwenye runinga yako, ukaiona sura ya Nuru. Nilijikuta kikaoni na huyo Nuru, sema hilo ni jina la uhusika tu.

Mambo yanaendaje?

Nashukuru Mwenyezi Mungu anasaidia.

Huko utokeako mnatuzidi nini?

Nafikiri mbali na minazi, pia tumewazidi jua. Jamani linawaka kama vile limelipwa.

Nina desturi moja hivi kila ninapomhoji msanii anayetokea Pwani, huwa natamani sana kujua, anatokea eneo gani, alikozaliwa, alikolelewa, kasomea wapi na vijimambo kama hivyo?

Majina kwenye kitambulisho cha serikali ni Selestine Nyagha Kivuma. Mimi ni toto la Kitaita, nimezaliwa na kulelewa Mombasa. Toka chekechea hadi kidato nimesomea Malindi halafu baadaye nikajiunga na chuo kikuu cha Technical University of Mombasa kusomea uanahabari.

Halafu, nimependa ulivyoipanga bio yako kwenye Instagram. Unasema wewe ni mwigizaji, mfanyabiashara na mwanaharakati dhidi ya dawa za kulevya…

Eeh! Uigizaji wangu nafikiri unafahamika kupitia vipindi mbali mbali nilivyoigiza ikiwemo Pete. Kwenye ujasiriamali, nimewekeza kwenye biashara za msosi. Ninacho kibanda changu cha chakula kinachonipa riziki kando na uigizaji. Mbali na hayo sio wengi wanaofahamu kuwa mimi ni mwanaharakati dhidi ya mihadarati.

Ulitokeaje ukawa mwanaharakati wa aina hiyo?

Yalinikuta baba, yalinikuta. Kunaye mwanafamilia wetu mmoja ambaye aliathirika vibaya na matumizi ya mihadarati. Hii ikawa motisha na msukumo wa kupinga janga hili. Usitamani kuwa na mtu wa karibu mwathirika. Inatesa. Inaumiza.

Aisee pole sana

Nishapoa Asante.

Turudi kwenye maigizo, ni muda gani sasa kwenye gemu?

Nimeanza toka nikiwa Kidato cha Pili, 2011 mpaka leo.

Kwa miaka hiyo 11 wajivunia nini kwenye taaluma hii?

Vipo vitu vingi sana, ila kikubwa zaidi ni kuwa uigizaji ni ajira. Na kwenye ajira kuna riziki.

Unavalia uhusika wa Nuru kwenye tamthilia ya Pete, ulijipataje huko?

Kuna rafiki yangu mmoja alinipigia simu akinifahamisha kuwa kasikia kuna usahili wa Pete. Nilisita kidogo ila akanisisitizia twende na hata akanisindikiza. Kule nilijitahidi na Mungu ni mwema nilihitimu na kuwekwa kwenye hesabu. Ukawa ndio mwanzo wa Nuru.Kitabia yule Nuru na Selestina unahisi wanaendana au ni watu wawili tofauti?? Haha! Nampenda sana Nuru, nikimwangalia Nuru kwa asilimia hamsini namuona Selestinah. Kuna wakati nilikuwa napewa vipande vya Nuru ambavyo viliendana kabisa na uhalisia wa maisha yangu.

Hapo kwenye maisha yako kihalisia, hivi umewahi kukutana na watu waliokuelewa visivyo kutokana na uhusika wako kama Nuru?? Kwa bahati nzuri au mbaya hapana. Wajua Nuru ni mhusika aliyeishia kupendwa sana na mashabiki. Sijawai kusomeka kwa ubaya.

Ukiachana na Pete ni kazi zipi zingine umetumika?? Kuna filamu ya Dr. Okossovo, ipo Series iitwayo Penzi halafu badaye ikaja hiyo Telenovela ya Pete ambayo nimekuwa mhusika kwa miaka minne.

Kwenye pete tunamwona Nuru na Jasiri wakihangaishana kwenye mapenzi, naomba nikuulize hivi Selestina umewahi kuhangaishwa na penzi?

Haha! Naamini hakuna aliyependa na akakosa kuhangaishwa na mapenzi hata kwa asilimia ndogo. Ndio uhalisia wa maisha yetu wanadamu. Kama hujawahi tendwa basi hujawahi penda.

Nuru anampenda mwanaume wa taipu ya Jasiri, Selestina anampenda mwanaume wa taipu gani vile?

Kwa kizazi hiki cha sasa, sasaivi nazingatia sana mwanamume mcha Mungu.

Nina imani ukimpata mwanaume anayemwogopa na kumheshimu Mungu inakua rahisi kukuheshimu pia wewe kama mwanamke. Pia ajue kunidekeza. Kingine awe mchapa kazi.

Hivi tukio kama la Angelina Jolie na Brad Pitt limewahi kukuta? Nahisi unafahamu kuwa mastaa hao waliotesha penzi lao walipokutana kwenye seti ya Mr & Mrs Smith.

Haha! Mmmh! Duh! Hili nalo linatokea wapi jamani. Mapenzi bwana wewe yaache tu.

Shangazi, mbona umenyong’onyea, litakuwa limeshakukuta wewe sababu hujanijibu?

Haha! Unachimba sana wewe. Kuwa mpole.

Haya basi ila utaniruhusu nizidi kuwa mzushi. Naomba uniambie kitu, hivi umewahi kuvunjwa mtima na bratha-kaka, kisha mawazoni ukahisi ni kama vile karma analipiza kisasi?

Jamani sikujua kikao kitakuwa cha kichokozi. Mmh! Sijawahi kuwaza kwa upande huo ila kwa kuwa umenitamkia, nimeanza kuhisi itakuwa ni Karma kweli hehe!

Kwa watu uliofanikiwa kudeti, hapo ulipo mapenzi kwako unayachukuliaje?

Kusema ukweli mimi ni mlevi wa mapenzi. Nayapenda mapenzi . Ni hisia nzuri kuwa na mtu umpendaye kando yako. Tatizo kumpata sasa Weeh! Sawa na kukesha ukipanda michongoma.

Wajua juzi, nikitia stori na dada mmoja mwigizaji aliniambia, katika maisha ya sasa ni poa wanawake waukubali ukweli mchungu kwamba wanaume, ni wa kuchangiana. Eti hamna mwanamume wa mwanamke mmoja. Hili linakuingiaje kichwani?

Hapo ndio wanawake tunapokosea. Mimi naamini kila mwanamke ana haki ya kumpata lazizi wake mmoja na akatulia naye. Kwa wanaume hii ni mitazamo tu potovu, kwa sababu kama kweli ni jambo la kukubalika mbona basi wajifiche. Wafanye hadharani. Wanaficha maana nafsi zao zinawasuta, wanajua sio sawa.

Kuna post moja ya ua la waridi likinyauka, uliloposti Februari 21, 2022 bila ya maelezo. Ukafunga eneo la watu kumimina komenti. Maanake nini?

Uliicheki posti vizuri. Posti ilijielezea haikuhitaji ufafanuzi wowote. Na niliziba komenti sababu sikuhitaji maoni au mitazamo ya mtu yeyote.

Khuh! Kweli Diamond aliimba, haya mapenzi bwana hayana maana…

Oya! Unaona sasa mitazamo kama hii, watu kama wewe ndio niliwazibia komenti.

Haha! Sina neno bibiye. Natania tu.

Mmh!

Bado nikigandia hapo Insta, kuna posti nyingine nikitafsiri kwa kunukuu ilisomeka ‘Kizazi chetu hichi ni cha huzuni tu, ila tuna picha nyingi za kufurahisha’.

Kila mtu kwenye mitandao posti zake huashiria furaha kwa asilimia kubwa. Lakini nyuma ya pazia utakuta mtu anapambana na changamoto kibao za kimaisha. Mitandaoni tunaogopa kuwa wakweli kwa kuhofia mitazamo na kuhukumiwa. Kwa maana hiyo tunalazimika kuhadaa mitandaoni mutakabala wa maisha halisi.

Binadamu hupanga ila Mungu huamua, Selestina kwa miezi iliyosalia mwaka huu, umejipangaje kisanii?

Kwa sasa nimesita kidogo sababu tushamaliza kushuti Pete. Nimeelekeza nguvu zote kwenye kibanda changu kwa sasa. Ikitokea kazi nyingine ya uigizaji, nitachangamka. Sitasita kuwafahamisha mashabiki wangu wakae mkao wa kula.

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Tutathmini upya mchakato mzima wa kuomboleza...

KASHESHE: ‘Chibu’ huyoo…azidi kupepea

T L