Makala

KIPWANI: ‘Wasubiri bonge la surprise Krismasi’

October 4th, 2019 2 min read

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

JUAN Mutua ni miongoni mwa wale wanaoamini ikiwa sehemu uliyoko haina nyota nawe, ni muhimu na vizuri kubadilisha upepo kwa kuguria kwingine.

Tangu amalize masomo yake ya sekondari huko Makueni mnamo mwaka 2017, Mutua al-maarufu Dema Boy alifanya bidii zake zote za kuendeleza kipaji cha uimbaji wake lakini wapi, aliambulia patupu.

Mnamo mwaka 2018, alimsaka shangaziye anayeishi Mwatate kule Taita ili kuishi naye kujaribu kukipalilia kipaji chake.

“Namshukuru shangazi kwa kunipokea kwani tangu nifike hapa Mwatate mwaka mmoja uliopita, nimeona grafu yangu ya muziki ikipanda kwa kasi,” asema Dema Boy.

Muziki ulianzia wapi?

Dema Boy: Nilikuwa mwimbaji tangu niko shule ya upili nikishiriki mashindano ya Tamasha za Muziki katika kitengo cha nyimbo za kizalendo. Hapo ndipo mshawasha wa kuendeleza kipaji hiki ulianza kukita mizizi na nilipomaliza masomo ulizidi kunikuna.

Hivyo basi bado waimba ngoma za kizalendo?

Dema Boy: La hasha! Niliziacha nyimbo hizo shule kwani hata nilipokuwa sijamaliza masomo yangu, azma yangu kubwa ilikuwa ni kuwa mwimbaji wa nyimbo za kisasa.

Na tangu ukamilishe elimu ya shule, umeachia kibao chochote?

Dema Boy: Naam! Kibao changu cha kwanza Kwachu nilikiachia mapema mwaka huu ila kikabuma. Hakikupokelewa nilivyotarajia lakini si kukata tamaa na ndio sababu bado napambana. Na mpaka sasa nimeweza kuachia vibao vingine viwili; Sema Nami Mashallah na Singizie (ambao una video pia).

Unatumia mitindo gani na kwa nini?

Dema Boy: Kwa kuwa ni majirani sana na Tanzania, natumia Bongo Flava niweze kunasa mashabiki wa pande zote mbili.

Una yeyote uliyeswalitika naye kimapenzi?

Dema Boy: Ndio ninaye tena ni mmoja pekee na wengine wawe karibu nami kimuziki sio mengineyo maana tumeamua tutabanana hadi mwisho.

Wawahusudu wanamuziki gani hapa nchini na ng’ambo?

Dema Boy: Hapa nchini nawapenda kina Susumila na Otile Brown. Nje ya nchi ninamshabikia Mbosso.

Unalenga kufikia wapi kimuziki?

Dema Boy: Haja yangu ni kukubalika hapa barani Afrika na Majuu.

Wazazi wako radhi wewe kuwa mwanamuziki?

Dema Boy: Walipinga sana hapo awali lakini baada ya kuvisikia vibao vyangu, wamenikubalia.

Unawaambia nini mashabiki wa muziki wako?

Dema Boy: Nawashukuru sana, waendelee kunishabikia na nawaomba waendelee kunipa sapoti.

Umewatayarishia nini sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya?

Dema Boy: Ninataka kuwapa ‘surprise’. Nitakachowapa kitakuwa zawadi bora ya sikukuu hizo mbili.