Michezo

Kipyegon na Cheruiyot kunogesha Wanda Diamond League

July 24th, 2020 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

BINGWA wa Olimpiki katika mbio za mita 1,500 Faith Chepng’etich Kipyegon na mfalme wa dunia katika mbio za mita 1,500 Timothy Cheruiyot wamethibitishwa kuwa sehemu ya wanariadha watakaonogesha duru ya kwanza ya mbio za Wanda Diamond League mnamo Agosti 14, 2020 jijini Monaco, Ufaransa.

Kipyegon ambaye atakuwa akitifua kivumbi cha Diamond League kwa mara ya kwanza katika historia, atatoana jasho na bingwa wa dunia katika mbio za mita 800 Halimah Nakaayi kutoka Uganda na nyota wa bara Ulaya katika mbio za mita 1,500 Laura Muir ambaye ni mzawa wa Uingereza.

Itakuwa mara ya kwanza kwa Kipyegon kushiriki mbio za kimataifa tangu alipojizolea nishani ya fedha katika mbio za mita 1,500 kwenye Riadha za Dunia zilizoandaliwa jijini Doha, Qatar mnamo 2019. Kipyegon alisajili muda wa dakika 3:54.22 nchini Doha na kuridhika na nafasi ya pili nyuma ya Sifan Hassan wa Uholanzi aliyejitwalia dhahabu baada ya muda wa dakika 3:51.95. Mgongo wa Kipyegon ulifuatwa kwa karibu na Mwethiopia Gudaf Tsegay (3:54.38).

Kwa upande wake, Cheruiyot alitamalaki mbio zake jijini Doha kwa muda wa dakika 3:29.26 mbele ya Taoufik Makhloufi wa Algeria (3:31.38) na Marcin Lewandowski kutoka Poland (3:31.46).

Cheruiyot ambaye ni bingwa mara tatu wa mashindano ya Diamond League, atapata fursa ya kurejesha hadhi yake katika mbio za mita 1,500 na  kulipiza kisasi dhidi ya kaka watatu wazawa wa Norway, Jakob, Filip na Henrik Ingebrigtsen.

Kaka hao watatu walimlemea Cheruiyot na Wakenya wenzake Elijah Manangoi, Edward Meli, Vincent Keter na Timothy Sein katika mbio za mita 2,000 za Maurie Plant Memorial zilizoandaliwa sambamba katika uwanja wa Nyayo Nairobi na jijini Oslo, Norway mnamo Juni 11, 2020.

Cheruiyot na Kipyegon wanakuwa katika kundi la pili la wanariadha wa humu nchini kuthibitishwa kunogesha kivumbi kijacho cha Diamond League baada ya bingwa wa dunia katika mbio za mita 5,000 kwa upande wa wanawake, Hellen Obiri na mfalme wa dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji Conseslus Kipruto.

Wanne hao ni wanariadha wa kwanza kupata vibali na pasipoti za Schengen zinazowakubalia kusafiri katika mataifa tofauti ya Muungano wa Bara Ulaya (EU) kwa minajili ya kushiriki mashindano mbalimbali yatakayoandaliwa kuanzia mwezi ujao.

Obiri ambaye pia ni bingwa wa Jumuiya ya Madola na malkia wa Afrika katika mbio za mita 5,000, atapania kutumia kivumbi cha Diamond League kuandikisha muda bora zaidi kuliko ule wa dakika 14:26.72 aliotumia kujinyakulia nishani ya dhahabu katika Riadha za Dunia za 2019 jijini Doha, Qatar.

Hata hivyo, atalazimika kukabiliana na ushindani mkali kutoka kwa mwanariadha matata mzawa wa Ethiopia na raia wa Uholanzi, Sifan Hassan aliyetawala mbio za mita 10,000 katika Riadha za Dunia mwaka jana kwa muda wa dakika 30:17.62.

Hassan, 27, alijishindia pia dhahabu katika mbio za mita 1,500 jijini Doha kwa muda wa dakika 3:51.95 na kuweka rekodi ya kuwa mtimkaji wa kwanza kuwahi kutamalaki fani za mbio hizo mbili katika makala moja ya Riadha za Dunia.

Kwa upande wake, Kipruto ambaye pia ni bingwa wa Olimpiki katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji, atalenga kuendeleza babe uliomzolea medali ya dhahabu mwaka jana nchini Qatar. Aliibuka mshindi baada ya muda wa dakika 8:01.35.

Bingwa wa dunia katika mbio za mita 1,500 Timothy Cheruiyot, mfalme wa Jumuiya ya Madola Elijah Manangoi, Timothy Sein, Winny Chebet na Vincent Keter wanaonolewa kwa sasa na kocha Bernard Ouma, ni miongoni mwa Wakenya wengine wanaotazamiwa kupata vibali vya kunogesha duru ijayo ya Damond League nchini Ufaransa.

Waziri wa Michezo, Amina Mohammed, amewaondolea wanariadha wote wa Kenya hofu ya kutupwa nje ya mbio hizo kwa kusisitiza kwamba Serikali na Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) zinaendelea kushawishi balozi mbalimbali za nchi zilizopo chini ya uvuli wa EU kuwapa wahusika vibali vya kushiriki mashindano hayo na mengine yatakayofanyika kuanzia Agosti.

Kenya ni miongoni mwa mataifa yaliyoachwa nje ya orodha ya nchi 15 za kwanza ambazo raia wao walipewa idhini ya kuzuru mataifa 26 ya bara Ulaya kuanzia mwezi huu wa Julai.

Watimkaji wa Kenya hawakujumuishwa pia katika ratiba ya awali iliyotolewa na waandalizi wa Diamond League jijini Monaco, Ufaransa mnamo Agosti 14.

Wanariadha Joshua Cheptegei wa Uganda na Hassan wa Uholanzi, ambao ni wapinzani wakuu wa Wakenya katika mbio za mita 10,000 kwa upande wa wanaume na wanawake mtawalia, wamo katika ratiba hiyo. Wawili hao watatifua kivumbi katika mbio za mita 5,000 kwa upande wa wanaume na wanawake mtawalia.

Mbali na Monaco, duru nyinginezo za Diamond League zilizotarajiwa kufanyika bara Ulaya msimu huu ni Stockholm (Uswidi) mnamo Agosti 23 na Brussels (Ubelgiji) mnamo Septemba 4.

Nyinginezo ni Roma/Naples (Italia) mnamo Septemba 17 na Gateshead (Uingereza) mnamo Septemba 26.

Tayari duru ya Paris iliyokuwa ifanyike Septemba 6 na mbio za Prefontaine Classic zilizoratibiwa kutifuliwa Septemba 20 zimefutiliwa mbali.