Michezo

Kipyegon, Obiri, Cheruiyot na Kipruto kuongoza Wakenya katika Doha Diamond League

September 23rd, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

BINGWA wa Olimpiki katika mbio za mita 1,500 Faith Kipyegon atakuwa akifukuzia ushindi wake wa nne kwenye mashindano ya Wanda Diamond League msimu huu atakaposhiriki mbio za mita 800 kwenye duru ya Doha, Qatar mnamo Septemba 25, 2020.

Kipyegon, 26, alitamalaki mbio za mita 1,000 (dakika 2:29.32) jijini Monaco, Ufaransa mnamo Agosti 14 kabla ya kuandikisha muda wa dakika 2:29.92 katika mbio hizi za mizunguko miwili na nusu jijini Brussels, Ubelgiji mnamo Septemba 4.

Katika duru hizo, Kipyegon alikuwa pua na mdomo kuvunja rekodi ya dunia ya dakika 2:28.98 iliyowekwa na Mrusi Svetlana Masterkova katika mbio za mita 1,000 mnamo 1996.

Alirejea kushiriki fani aliyoizoea ya mita 1,500 jijini Ostrava kwenye Riadha za Dunia za Continental Gold Tour zilizoandaliwa katika uwanja wa Mestky, Jamhuri ya Czech mnamo Septemba 8.

Alikosa mshindani wa kumtoa jasho katika mbio hizo alizozikamilisha kwa muda wa dakika 3:59.05 na kufuta rekodi ya dakika 4:00.96 iliyowekwa na raia wa Ethiopia Gudaf Tsegay mnamo 2017.

Japo Kipyegon anapigiwa upatu wa kuwika jijini Doha, atakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Wakenya Emily Cherotich na Eunice Sum ambaye ni bingwa wa zamani wa dunia katika mbio za mita 800.

Mbio hizo za mizunguko miwili zimevutia pia Winnie Nanyondo wa Uganda, Mwethiopia Alemu Habitam na Angelika Cichocka wa Poland.

Bingwa wa dunia katika mbio za mita 1,500 Timothy Cheruiyot atashiriki mbio za mita 800 kwa upande wa wanaume jijini Doha. Nyota huyo aliweka muda bora wa dakika 3:28.45 jijini Monaco kabla ya kutamalaki duru ya Stockholm, Uswidi (3:30.25) mnamo Agosti 23 katika mita 1,500. Atakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Wakenya Ferguson Rotich na Wycliffe Kinyamal, Erik Sowinski wa Amerika na Mwingereza Giles Elliot.

Rotich aliibuka mshindi wa nishani ya shaba katika mbio za mita 800 kwenye Riadha za Dunia zilizoandaliwa jijini Doha, Qatar mnamo 2019. Alitupwa hadi nafasi ya nane katika duru ya Diamond League jijini Monaco (1:45.48) kabla ya kujinyanyua na kuambulia nafasi ya nne (1:45.11) jijini Stockholm.

Bingwa wa Dunia na Jumuiya ya Madola katika mbio za kta 5,000 Hellen Obiri atalenga pia kujinyanyua baada ya kusajili matokeo mseto katika duru za Monaco na Stockholm. Obiri aliibuka mshindi wa mbio hizo za mizunguko 12 kwa muda wa dakika 14:22.12 jijini Monaco kabla ya kurushwa katika nafasi ya 11 kwenye mbio za mita 1,500 (4:10.53) jijini Stockholm.

Atashiriki mbio za mita 3,000 jijini Doha ambapo atatoana jasho na bingwa wa dunia na mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na vidimbwi vya maji, Beatrice Chepkoech.

Kivumbi hicho kimevutia pia Qualyne Kiprop, bingwa wa Afrika katika mbio za mita 1,500 Winny Chebet, bingwa wa dunia katika mbio za mita 5,000 kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 Beatrice Chebet, mshindi wa nishani ya shaba katika mbio za mita 10,000 duniani Agnes Tirop na bingwa wa zamani wa dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji Hyvin Kiyeng.

Wakenya hawa watapania kubwaga Waethiopia Tsegay Gudaf na Hailu Lemlem na Waingereza Laura Weightman na Eilish Mcolgan.

Bingwa wa Olimpiki na dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji, Conseslus Kipruto atarejea ulingoni kwa mara ya kwanza baada ya kupona Covid-19.

Mtimkaji huyo atanogesha mbio za mita 1,500 kwa pamoja na Wakenya wenzake Vincent Kibet, Brimin Kiprono na Bethwell Birgen. Mbio hizo zimevutia pia Waethiopia Selemon Barega na Lamecha Girma pamoja na Soufiane El Bakkali wa Morocco.