Kiraitu aapa kuangusha Mbunge uchaguzini ubabe kati yake na Munya ukizidi

Kiraitu aapa kuangusha Mbunge uchaguzini ubabe kati yake na Munya ukizidi

NA GITONGA MARETE

GAVANA Kiraitu Murungi ameapa kuendesha kampeni ya kumpinga vikali Mbunge wa Afrika Mashariki, Mpuru Aburi ili asishinde kiti cha ubunge huku uhasama ukitokota ndani ya vyama tanzu vya muungano wa Azimio la Umoja One Kenya kaunti ya Meru.

Uhasama huo ni wa aina yake kwa kuwa wanaopingana hawagombei kiti kimoja kwa tikiti ya vyama tanzu vya Azimio lakini unasababishwa na vita vya ubabe kati ya Bw Murungi na Waziri wa Kilimo Peter Munya.

Hii imefanya washirika wa Bw Murungi kuonya Bw Munya kwamba, wadhifa wa uwaziri alioahidiwa sio lazima aupate, hatua inayopandisha joto la kisiasa siku 40 kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Bw Aburi anamezea mate kiti cha eneobunge la Tigania Mashariki alichopoteza kwa Bw Gichunge Kabeabea mnamo 2017.

Bw Kabeabea anatetea kiti hicho kwa tikiti ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) cha Naibu Rais, William Ruto huku Bw Aburi akigombea kwa chama chake cha National Ordinary Peoples Empowerment Union (NoPEU) party.

Bw Murungi anamlaumu Bw Aburi kwa kumuunga mkono mpinzani wake mwakilishi wa kike Kawira Mwangaza (Independent) badala ya kumuunga yeye katika muungano wa Azimio ambao mgombea urais wake ni Raila Odinga.

Akiwa katika mkutano wa kampeni katika soko la Kariene, Imenti ya Kati wiki jana, mbele ya Bw Munya, Bw Aburi aliwataka wakazi kumpigia kura Bi Mwangaza, matamshi ambayo yalimkasirisha Bw Murungi aliyeshangaa kwa nini Bw Aburi hampigii debe ilhali wote wamo ndani ya Azimio.

Bw Munya pia aliambia wakazi kwamba hakuna ushindani katika kura za urais, akiongeza kuwa: “Katika kiwango cha ugavana na viti vingine, tutaamua tutakayepigia kura.”

Mnamo Jumatano, Gavana Murungi alijibu: “Sasa kila mwanasiasa yuko kivyake huku tukiunga Raila sisi sote. Mpuru anampigia debe Kawira na tunajua ni kipaza sauti wa Bw Munya hivi kwamba, kile waziri huyo hawezi kusema ni Mpuru anayemsemea. Nimeamua kumuunga Kabeabea na nitahakikisha Mpuru hatashinda kiti cha kisiasa Meru baada ya Agosti 9.”

Tangazo lake limepokelewa kwa mshangao huku wadadisi wakisema linaweza kuathiri muungano wa Azimio katika eneo hilo ambalo ni ngome ya UDA.

  • Tags

You can share this post!

Mjukuu wa Moi aandamwa na mke waliyetalikiana agharimie...

TAHARIRI: IEBC isikubali presha za mirengo, ifuate sheria

T L