Kiraitu atakiwa kulipa Sh274m kabla ya kukabidhiwa chama

Kiraitu atakiwa kulipa Sh274m kabla ya kukabidhiwa chama

Na GITONGA MARETE

WANASIASA sasa wanatumia mamilioni ya fedha kununua vyama kujiandaa kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao.

Wengi wa wanasiasa hao wanahofia kuwa huenda wakanyimwa tiketi na vyama vikubwa hivyo.

Mzozo unaohusu umiliki wa chama cha Restore and Rebuild Kenya (RBK), umeanika hayo, baada ya Katibu mpya wa chama hicho kinachofahamika sasa kama Devolution Empowerment Party (DEP), Bw Mugambi Imanyara, kudai kuwa walitakiwa kulipa Sh274 milioni ili kupewa chama hicho.

Chama hicho cha DEP kinahususishwa na Gavana wa Meru Kiraitu Murungi, ambaye analenga kukitumia kutawala siasa za Mlima Kenya Mashariki hasa kaunti za Tharaka-Nithi, Embu na Meru.

Kuhusu mzozo wa RBK, wanachama wawili Aloysius Okoth Mondoh na Peter Gordon Ochieng Odeng’, wamepinga kuchukuliwa kwa chama hicho na Bw Murungi anayelenga kukitumia kutetea kiti chake cha ugavana mnamo 2022.

Hata hivyo, stakabadhi za korti zinaonyesha kuwa Bw Imanyara aliwasilisha kesi katika Jopo la Kutatua Mizozo ya Vyama vya Kisiasa (PPDRT), akidai Bw Mondoh aliitisha Sh274 milioni kabla ya kuachilia udhibiti wa RBK.

“Baada ya kukataa kumpa pesa hizo aliapa kuwa hatungechukua usimamizi wa chama,” akasema Bw Imanyara kwenye stakabadhi za korti.

Alishikilia kuwa Bw Murungi hawezi kuchukua usimamizi wa chama hicho bure.

Kesi hiyo itatajwa kesho ambapo PPDRT inatarajiwa kutoa mwelekeo zaidi.

You can share this post!

Seneta taabani tena kwa dai la kujeruhi mwanamke

Familia ya Masten Wanjala yamkana, mwili wasalia mochari

F M