Michezo

Kirui na Rono waanika maazimio yao kwenye Valencia Marathon

November 30th, 2020 4 min read

Na CHRIS ADUNGO

BINGWA mara mbili wa dunia katika mbio za marathon, Abel Kirui amejiwekea malengo ya kuwa miongoni mwa wanariadha watakaokamilisha mashindano yajayo ya Valencia Marathon katika nafasi tatu za kwanza.

Kirui atakuwa akinogesha kivumbi hicho cha Disemba 6, 2020 akitazamia kuboresha zaidi muda wake baada ya kukosa fursa ya kushiriki Amsterdam Marathon iliyofutiliwa mbali msimu huu kwa sababu ya janga la corona.

“Tumekuwa tukilalamika sana msimu huu kwa sababu ya kukosekana kwa mashindano. Sasa nafasi ndiyo hii imejipa. Nitapania kuichangamkia vilivyo na kuwa miongoni mwa washindi wa medali katika mbio za Valencia Marathon,” akasema.

Hata hivyo, anahofia kwamba hajajiandaa vya kutosha kwa mbio hizo ikizingatiwa kwamba alijumuishwa kwenye orodha ya washiriki wiki kadhaa baada ya wenzake kuanza mazoezi ya kiwango cha juu.

“Hizi ni mbio za haiba kubwa zitakazotawaliwa na ushindani mkali. Kila mwanariadha atakayekuwa nchini Uhispania kwa kivumbi hiki atakuwa amejiandaa vya kutosha kwa kuwa wengi wao walianza kufanya mazoezi mapema. Tutarajie makuu,” akasema Kirui aliyeshinda mbio za marathon kwenye Olimpiki za London mnamo 2012.

Licha ya kutoshiriki mashindano mbalimbali ya haiba kubwa kwa kipindi kirefu, Kirui amesisitiza kwamba anajivunia tajriba pevu ambayo itamwezesha kuwazidi ujanja wapinzani wake. Mwanariadha huyo aliibuka mshindi wa marathon duniani mnamo 2009 jijini Berlin, Ujerumani na kutetea taji hilo kwa mafanikio mnamo 2011 jijini Daegu, Korea Kusini.

Mnamo 2016, aliibuka mshindi wa mbio za Chicago Marathon kabla ya kuambulia nafasi ya pili kwenye mbio hizo mnamo 2017.

Mbali na Kirui, mwanariadha mwingine anayetarajia kunogesha pakubwa mbio za Valencia Marathon ni mshindi mara mbili wa Toronto Marathon, Philemon Rono aliyekosa kivumbi cha Boston Marathon baada ya mbio hizo kufutiliwa mbali kwa sababu ya corona.

Rono ambaye amekuwa akijindalia katika eneo la Kaptagat ni mwingi wa matumaini kwamba ataibuka mshindi wa Valencia Marathon ikizingatiwa ukubwa wa kiwango cha maandalizi ambayo amefanya.

“Mbio za Valencia zitakuwa zangu za kwanza kushiriki baada ya Toronto Marathon mnamo 2019. Nimejiandaa vya kutosha na sioni sababu ya kutotawala kivumbi hicho na hatimaye kuendea nishani ya dhahabu,” akasema Rono almaarufu ‘Small Police’.

Rono aliibuka mshindi wa Toronto Marathon mnamo 2017 kabla ya Benson Kipruto kumpokonya taji hilo mnamo 2018. Hata hivyo, alirejea ulingoni kwa matao ya juu na kulitwaa tena mnamo 2019.

Mbali na Kirui na Rono, Kenya itawakilishwa pia na Geoffrey Kirui, Daniel Kemboi, Lani Rutto, Evans Chebet, Reuben Kiprop na Lawrence Cherono aliyeibuka mshindi wa Chicago Marathon mnamo 2019.

Watatoana jasho na Waethiopia Birhanu Legese anayejivunia muda wa tatu wa kasi zaidi kwenye historia ya marathon, Kinde Atanaw ambaye ni bingwa mtetezi wa Valencia Marathon, bingwa wa dunia Lelisa Desisa na Leul Gebreselasie aliyejizolea dhahabu ya Valencia Marathon mnamo 2018 (2:04:02).

Mbio hizo zimevutia jumla ya wanaume 21 wanaojivunia muda bora wa chini ya saa 2:07 kwenye mashindano ya awali.

Katika kategoria ya mbio za Valencia Half Marathon, Kenya itawakilishwa na mshikilizi wa nishani ya shaba katika mbio za mita 10,000 duniani, Rhonex Kipruto.

Kipruto, 21, atakuwa akishiriki kivumbi cha nusu marathon kwa mara ya kwanza baada ya kuweka rekodi ya dakika 26:24 kwenye mbio za barabarani za kilomita 10 jijini Valencia mnamo Januari 12 mwaka huu.

Washindani wake wakuu kwenye mbio hizo watakuwa mshindi wa nishani ya fedha kwenye Nusu Marathon za Dunia, Kibiwott Kandie na bingwa mara mbili wa medali ya shaba kwenye marathon duniani, Bedan Karoki. Watatu hao wataenyana na Mganda Jacob Kiplimo aliyeibuka mshindi wa mbio za dunia za Nusu Marathon mnamo Oktoba nchini Poland (dakika 58:49).

Kwa upande wa wanawake, Sheila Chepkirui anapigiwa upatu wa kutawala mbio hizo za kilomita 21 ambazo pia zimevutia Wakenya Dorcas Tuitoek na Brenda Jepleting.

Raia wa Ethiopia, Letesenbet Gidey aliyeweka rekodi mpya ya dunia katika mbio za mita 5,000 mapema mwaka 2020 atakuwa akishiriki mbio za nusu marathon kwa mara ya kwanza. Atatoana jasho na wenzake Genzebe Dibaba ambaye ni mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za mita 1,500 na Senbere Teferi aliyeshinda nishani ya fedha katika mbio za mita 5,000 duniani mnamo 2015 kabla ya kusajili muda bora wa saa 1:05:32 kwenye Valencia Half Marathon mnamo 2019.

Mbio za kilomita 21 na 42 jijini Valencia, Uhispania zimevutia zaidi ya wanariadha 100 kutoka mataifa 43 tofauti. Katika miaka ya hivi karibuni, jiji la Valencia limekuwa jukwaa maridhawa kwa wanariadha kuvunja baadhi ya rekodi kwenye mbio za masafa marefu za kilomita 21 na 42.

Mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za Nusu Marathon, Peres Jepchirchir amesema ana kiu ya kufunga rasmi kampeni za riadha msimu huu kwa ubingwa wa taji la Valencia Marathon.

Mtimkaji huyo atajitosa ulingoni kwa minajili ya mbio hizo wiki saba baada ya kuibuka mshindi wa makala ya 24 ya mbio za dunia za Nusu Marathon zilizofanyika jijini Gdynia, Poland mnamo Oktoba 17, 2020.

Jepchirchir aliyeweka rekodi mpya ya dunia ya saa 1:05:16 wakati huo, atakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Wakenya Purity Rionoripo, Fancy Chemutai na mshikilizi wa zamani wa rekodi ya dunia katika nusu marathon, Joycline Jepkosgei. Itakuwa mara ya kwanza kwa Chemutai kutifua kivumbi cha kilomita 42.

“Natazamia msimu wangu ukamilike kwa upekee zaidi – kwa taji la Valencia Marathon ambalo nalenga kulitwaa kwa muda wa saa 2:17 au saa 2:18 hivi,” akasema Jepchirchir.

Kwa upande wake, Jepkosgei ameapa kutumia mbio hizo kama jukwaa zuri la kujinyanyua na kudhihirisha ubabe wake baada ya kuambilia nafasi ya sita kwa muda wa saa 1:05:58 kwenye Nusu Marathon ya Dunia nchini Poland mwezi jana.

“Niko katika hali shwari na mashabiki wana kila sababu ya kutarajia makuu kutoka kwangu. Tutazamie kivumbi kikali,” akasema Jepkosgei.

Wanne hao watakaowakilisha Kenya kwa upande wa wanawake watalazimika kutoana jasho na Mwethiopia Birhane Dibaba. Mbio hizo zimevutia wanariadha 17 wa kike wanaojivunia muda bora wa chini ya saa 2:24 kwenye mashindano mbalimbali ya awali.

Mbali na Mjerumani Melat Kejeta aliyejizolea nishani ya fedha kwenye Riadha za Dunia za 2019 jijini Doha, Qatar, mbio za Valencia Marathon zitanogeshwa pia na Mwethiopia Ruti Aga aliyeibuka bingwa wa Tokyo Marathon mnamo 2019 (2:18:34).