Habari za Kaunti

Kisa cha Kagombe na ufyatuaji wa risasi za mauti

May 18th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

MBUNGE wa Gatundu Kusini Bw Gabriel Kagombe anasakwa na maafisa wa Idara ya Uchunguzi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa tuhuma za kuua na kujeruhi kwa risasi alipojipata katika mshikemshike wa kisiasa Thika Mjini mnamo Ijumaa.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Kiambu Bw Michael Muchiri, mtu mmoja aliaga dunia huku wengine kadhaa wakipata majeraha.

Hii ni licha ya Mbunge wa Githunguri Bi Gathoni Wamuchomba kudai kwamba walioaga dunia ni wawili.

Bw Muchiri alisema kwamba kisa hicho kilitokea katika mtaa wa Kiganjo ulioko Thika Mjini katika hafla ya ufunguzi wa soko la umma.

Hafla hiyo ilikuwa imepangwa na Mbunge wa Thika Mjini Bi Alice Ng’ang’a huku akipigwa jeki na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Bw Kimani Ichung’wah na ambaye pia ni Mbunge wa Kikuyu.

Wengine katika hafla hiyo walikuwa ni Bw Kagombe na mwenzake wa Gatundu Kaskazini Bw Elijah Kururia.

Wote hao huwa na uhasama na gavana wa Kiambu Bw Kimani Wamatangi ambapo inadaiwa kwamba tofauti hizo zilizoishia mbunge Kagombe kuonekana hadharani akifyatua zaidi ya risasi 10, zote akilenga raia, ndizo zilikuwa zimejidhihirisha kwa ghasia.

“Ni suala ambalo tunalichunguza. Kwa sasa habari rasmi ni kwamba kuna mwanamume mmoja aliyeaga dunia. Haijulikani ni nani aliyemuua lakini kuna habari zinazochunguzwa kuhusu mbunge huyo na jinsi inavyodaiwa kwamba alitumia bastola yake. Kwa sasa anahitajika kuandikisha taarifa na idara ya DCI katika makao makuu yaliyo Kiambu Road,” akasema afisa mmoja ambaye hakutaka kutajwa akisema wakubwa wake wangetoa maelezo zaidi.

Gavana Wamatangi alikashifu “siasa za upuzi na uhalifu wa kuua raia kwa msingi wa kutwaa mamlaka ya wananchi ambayo hupeanwa tu kupitia upigaji kura katika uchaguzi”.

“Kufika awamu ya siasa ambapo watu wataenda kwa soko wakitaka kujinyakulia mamlaka ya kisiasa kupitia kuua wapigakura wanaowapinga, ni ishara tosha kwamba kuna hatari kubwa inayofaa kusakamwa kabla haijageuka kuwa mauaji ya halaiki,” Bw Wamatangi alisema.

Alisema kwamba siasa za ugaidi zimejipa mizizi katika Kaunti ya Kiambu na ni lazima vitengo vya usalama sasa viwajibike kabla ya hali hiyo kugeuka kuwa hatari zaidi ikizingatiwa vyeo vya wahusika.

Hayo yakijiri, Bw Kagombe aliweka picha kwa mitandao ya kijamii akiwa amelazwa hospitalini kwa madai kwamba alishambuliwa na genge la vijana katika mkutano huo.

Mbunge wa Gatundu Kusini Bw Gabriel Kagombe akiwa hospitalini. PICHA | HISANI

Duru za polisi zilifichulia Taifa Leo kwamba kuna wanasiasa watatu ambao walikuwa wametiwa mbaroni katika kisa hicho “lakini simu za wenye ushawishi serikalini zikatushinikiza tuwaachilie”.

“Sisi polisi tulifika eneo hilo kwa haraka, tukashuhudia yote na hata tukasaidia kuokoa hali kupitia kurusha vitoa machozi na tukawakamata wabunge kadha lakini wakubwa wao wakatupigia simu wakitaka kwanza tuwaachilie,” kikadai chanzo hicho.

Bw Muchiri alisema kwamba hajui kuhusu kupigwa kwa Bw Kagombe kwa kuwa hakuna taarifa rasmi ambayo ameandikisha ya kuthibitisha hayo.

“Kesi zote kubwa kama hizo ni za kitengo cha DCI na ripoti tutazipata jinsi uchunguzi utakavyosonga,” akasema Bw Muchiri.

Bi Wamuchomba aliteta kwamba “wakati wengine wetu tulikuwa tumeenda kutetea watu wa Mlima Kenya katika Kongamano la Limuru III dhidi ya udhalimu wa serikali, nao wengine wa serikali hiyo walikuwa Kiganjo hali iliyosababisha watu wao kuawa”.

Baadhi ya wananchi waliokuwa katika hafla hiyo walisema kwamba waliona risasi zikifyatuliwa zikilenga umati wa watu na katika hali ya risasi njoo mguu niponye, kukawa na mauti na majeruhi.

Bw Muchiri alisema haki itahakikishwa imejidhihirisha katika kisa hicho.