Dondoo

Kisanga polo kufumania mganga akichovya asali yake

July 30th, 2018 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

Kibabii, Bungoma

Kalameni mmoja kutoka hapa, alimtimua mganga baada ya kubaini kwamba alikuwa paka asiyeachiwa maziwa.

Kulingana na mdokezi, polo alimualika mganga kwa boma lake amgangue mkewe. Duru zinasema mara kwa mara jamaa alikuwa akimuacha mganga na mkewe mgonjwa ili atibiwe.

Inasemekana mkewe alikuwa ametaabika mno kutokana na ugonjwa ambao haukujulikana na madaktari wa hospitali zote alizozuru.

“Polo aliamua kumtembelea mganga ambapo walisikilizana asafiri hadi kwa boma,,” alieleza mdokezi.

Penyenye zinasema polo alianza kupata fununu kwa majirani kwamba mganga alikuwa akichovya asali kabla ya kuanza kumtibu mkewe.

Inadaiwa siku ya tukio, polo alimdanganya mganga kwamba angerudi jioni. Alimsihi aendelee kumhudumia mkewe.

Jamaa alienda na kujificha kwa nyumba ya jirani.

Kulingana na mdokezi, mganga alianza shughuli zake naye jamaa akawa anachungulia kwa dirisha.

“Hakuamini alichoona. Mganga alikuwa juu ya mzinga akirina asali,” alieleza mdokezi.

Duru zinasema mganga aliangushiwa makofi kadhaa na polo.

“Ilikuwa ni leo pekee. Sijawahi kufanya hivyo tena. Tafadhali nisamehe,” mganga alimrai polo.

Majirani walimzomea mganga huku wakitoa siri zote za mganga huyo.

“Kila wakati huwa unajifungia ndani ya nyumba. Juzi uliwafukuza watoto waliokuwa wakicheza hapa,” jirani alidai.

Inasemekana ilibidi mganga kukiri kosa asiangamizwe. Kwa kusikia hivyo, polo alimpa mganga dakika tano afunganye virago na kuondoka.

Mganga alilazimika kutoroka mbio kwani alihofia gadhabu ya majirani.

Haikujulikana ikiwa baadaye polo alisikilizana na mkewe au la kuhusu kitendo alichofanya na mganga. Hadi wa leo haikujulikana ugonjwa aliougua mke wa jamaa huyo.