Michezo

Kisauni Hope FC yawainua vijana

June 6th, 2020 2 min read

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

KISAUNI Hope FC ni mojawapo ya klabu za soka ya vijana iliyofanikiwa kutoa chipukizi kadhaa waliofanikiwa kucheza kiwango cha kimataifa.

Chipukizi kadhaa wa klabu hiyo ya Kaunti ya Mombasa ambayo imeweza kutoa chipukizi kadhaa ambao wameweza kuchezea timu ya taifa ya Harambee Stars ya umri chini ya miaka 15 na ambao wamesafiri na timu hiyo kucheza mechi kadhaa nje ya nchi.

Ismail Ahmed ambaye ni kocha mkuu wa Kisauni Hope FC anajivunia kuona vijana wake wapatao wanne tayari wameingia katika daftari la kihistoria kuwa wanasoka wenye kutambulika sio hapa nchini bali hata nchi jirani ya Tanzania.

“Ninajivunia klabu yangu kuweza kuwafanikisha wanasoka wanne, mmoja anayechezea timu ya taifa ya vijana wa umri chini ya miaka 15, wawili wanaotarajiwa kwenda Ureno kwa ajili ya majaribio yanayodhaminiwa na aliyekuwa nahodha wa Real Madrid ya Uhispania, Luis Figo,” akasema Ahmed.

Mkufunzi huyo anasema anafurahishwa na straika Nyale Khamisi kuwa miongoni mwa wachezaji waliowakilisha nchi kwenye mashindano ya Cecafa U-15 Championship yaliyofanyika Eritrea mnamo Agosti 2019.

Pia anafurahia kutambuliwa kwa wanasoka wake wawili, William Gitama na Abubakar Fadhil almaarufu Kulola waliokuwa wamefanikiwa kwenda Ureno mwezi wa Aprili 2020 lakini janga la corona likatatiza mipango.

Ilikuwa wanasoka hao wawili waende huko Ureno kwa kipindi cha wiki mbili wakifanyiwa majaribio katika chuo kinachomilikiwa na Figo.

Ahmed amesema kuwa matunda yote hayo yamepatikana kutokana na juhudi zinazotekelezwa na katibu wa tawi la Pwani Kusini la Shirikisho la Soka nchini Kenya (FKF), Lilian Nandundu aliyemtaja kuwa kiongozi aliyesaidia pakubwa kuangazia soka ya vijana.

“Namshukuru Lilian kwa juhudi zake za kuhakikisha vijana wa Pwani wanapat fursa ya kuendeleza vipaji vyao sio hapa nchini pekee bali hata ng’ambo. Ni hakika amesaidia pakubwa kuhakikisha wanasoka wetu wazuri, wamepata fursa ya kuiwakilisha nchi yao,” akasema.

Ahmed anasema timu yake ya wachezaji wa miaka 16 na 17 wanashiriki kwenye Ligi ya Kaunti ya Mombasa inayosimamiwa na FKF Pwani Kusini na wanaendelea kupata uzoefu wa ligi hiyo ambayo timu nyingi wanachezesha wachezaji wa umri mkubwa.

Kocha wa Kisauni Hope FC, Ismail Ahmed. Picha/ Abdulrahman Sheriff

Kisauni Hope U-13 ilishinda taji la ligi hiyo kwa miaka ya 2017 na 2018 hali timu yake ya umri chini ya miaka 15 ilishiriki ligi na kuibuka mabingwa wa misimu hiyo miwili.

Kikosi cha Kisauni Hope U-16 kina Renson Wakalo (Nahodha), Abubakar Fadhili, William Gitama, Juma Khalid, Amani Juma, Mbarak Mussa, Fred Bidii, Carlos Mzungu na Nyale Khamisi.

Wengine ni Swaleh Fahim, Claus Mzungu, Athman Sorondo, Christopher Mwanza, Shukran Mohamed Abubakar Nyawa, Swabri Muhsin, Paul Geoffrey na Harith Said.

Meneja wa timu hiyo, Suheil Abdalla anasema kuwa wanajitahidi kutimiza wajibu mkubwa wa kuinua vipaji vya vijana wanaoinukia vizuri kisoka na akawaomba wahisani wajitokeze kuwasaidia kwa njia moja ama nyingine.

“Tunafanya bidii kuhakikisha vijana wa sehemu hii ya Kisauni wanashiriki kucheza kandanda badala ya kukaa mitaani bila ya kuwa na la kufanya. Udhamini utatusaidia kuinua haraka vipaji vingi ili mitaa yetu hii itoe wanasoka bora zaidi wakubwa na watoto wanaoinukia,” akasema Suheil.

Wachezaji waliochaguliwa kwenda huko Ureno wamesema wanasubiri kwa hamu wakati ufike ili wapate kwenda huko na wana matumaini makubwa wataweza kufuzu kuvutia maskauti wa klabu mbalimbali za barani Afrika.