Habari za Kaunti

Kisii yaruhusiwa kukusanya ushuru Keroka

April 10th, 2024 2 min read

NA RUTH MBULA

SERIKALI ya Kaunti ya Kisii imepata ushindi wa awamu ya kwanza baada ya majaji wa Mahakama ya Rufaa walioketi Kisumu kuamuru iendelee kukusanya ushuru katika mji wa mpakani wa Keroka.

Tangu mfumo wa ugatuzi uanze kutekelezwa 2013, Kaunti za Kisii na Nyamira zimekuwa zikizozania udhibiti wa mji huo ambao ni wa pili kwa ukubwa baada ya mji wa Kisii.

Majaji Hannah Okwengu, Ali-Aroni na Joel Ngugi mnamo Aprili 9, walisitisha utekelekezaji wa uamuzi wa Jaji wa Mahakama ya Ardhi na Mazingira Mugo Kamau kwamba serikali ya Kaunti ya Kisii isiendelea kukusanya ushuru katika mji huo.

“Baada ya kushauriana na mawakili wa pande zote inaamuliwa kuwa hali ilivyokuwa zamani idumishwe hadi rufaa hii itakaposikizwa na kuamuliwa,” likasema agizo la mahakama hiyo ya rufaa.

Majaji hao watatu walisema kuwa mzozo kuhusu Keroka “ni suala lenye umuhimu kwa umma.”

Waliamuru wahusika kuwasilisha taarifa zilizoandikwa ili kuwezesha kusikizwa kwa kesi yenye rufaa yenyewe.

Washtakiwa katika kesi hiyo nambari E026 YA 2024 ni diwani wa Rigoma Nyambega Gisesa, Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC), Mwanasheria Mkuu na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Wengine ni Serikali ya Kaunti ya Nyamira, na maafisa wa Idara ya Mipango katika Wizara ya Ardhi Barare Nyang’au, Francis Ndaburi na Charles Osoro Kiboi.

Keroka iko katika mpaka wa kaunti hizo mbili huku ramani za NLC, IEBC na hati ya utendakazi wa mji huo ulioanzishwa 2015 zikiwa stakabadhi zinazotumika katika mzozo huo.

Diwani Gisesa alielekea kortini 2023 akidai sehemu kubwa ya mji wa Keroka iko ndani ya Kaunti ya Nyamira.

Alilalamika kuwa wafanyabiashara katika mji huo wanatozwa ushuru mara dufu na serikali za kaunti za Kisii na Nyamira.

Katika uamuzi wake wa Februari 15 mwaka huu, Jaji Kamau aliamuru maafisa wa kaunti hizo mbili “kujikita ndani ya himaya zao wanapokusanya ushuru na ada nyinginezo.”

Jaji huyo alisema kuwa mipaka ya kaunti hizo mbili tayari ilikuwa imeainishwa.

“Ni rahisi zaidi kujua mahala ambapo mpaka kati ya Kaunti za Nyamira na Kisii upo,” akasema alipokuwa akitoa uamuzi kuhusu kesi hiyo.

Jaji Mugo alisema ni kinyume cha sheria kwa wafanyabiashara kutozwa ada mara dufu.

“Uamuzi unatolewa hapa kwamba kuwalazimisha wakazi wa Keroka kulipa kodi, ushuru na ada nyinginezo kwa Kaunti za Kisii na Nyamira ni sawa na kuhujumu haki zao za umiliki wa mali,” Jaji Mugo akasema.