Habari Mseto

Kisiki katika uchunguzi wa mkasa wa Nakumatt

March 14th, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

KUMESALIA mashahidi wanne katika uchunguzi wa kubaini kilichosababisha moto uliopelekea watu zaidi ya 20 kuteketea katika duka la Nakumatt, kiongozi wa mashtaka Solomon Naulikha alidokeza Jumanne.

Bw Naulikha alimweleza hakimu mkuu Francis Andayi kwamba afisa anayechunguza kesi hiyo alienda kazi kaunti ya Turkana na kwamba hajarudi.

Aliomba mahakama iahirishe kesi hiyo hadi  afisa huyo atakaporudi Nairobi.

Hata hivyo hakimu alimkashifu Bw Naulikha na kumweleza  uchunguzi huo ulikuwa uendelee na mashahidi wawili aliokuwa amesema wamesalia waeleze kilichojiri wakati wa mkasa huo wa moto miaka tisa iliyopita.

“Naomba radhi hatutaweza kuendelea mbele na uchunguzi huu wa mkasa wa moto wa duka la supa la Nakumatt. Afisa anayejua waliko mashahidi yuko kazini kaunti ya Turkana. Hatutaweza kuendelea. Naomba uchunguzi huu utengewe siku nyingine,” alisema Bw Naulikha.

Mahakama iliahirisha shughuli hiyo hadi wiki ya tatu ya  Aprili 2018.