Habari Mseto

Kisiki kipya kinachofanya aliyeteuliwa Naibu Gavana Kisii kusalia akimeza mate

April 6th, 2024 1 min read

NA WYCLIFFE NYABERI

GAVANA wa Kisii Simba Arati(pichani) atalazimika kusubiri kwa muda zaidi kabla ya chaguo lake la Bw Elijah Obebo kama naibu wake kuidhinishwa.

Hii ni baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kusema haiwezi kutangaza jina la Bw Obebo kwenye gazeti rasmi la serikali kwa kuwa taasisi hiyo kwa sasa haina mwenyekiti.

Kabla ya kuteuliwa kwake, Bw Obebo alikuwa mwenyekiti wa Bodi ya Kuwaajiri Wafanyakazi wa Kaunti (CPSB).

ODM, kupitia mwenyekiti wake wa Bodi Kuu Inayosimamia Chaguzi zake Catherine Mumma, ilimwandikia IEBC kuwasilisha jina la Bw Obebo kama mteule wa kiti hicho kilichobaki wazi kufuatia kung’atuliwa afisini kwa Dkt Robert Monda mwezi jana.

Chama hicho kilitaka Bw Obebo afanyiwe ukaguzi lakini Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC Marjan Hussein Marjan, akadokeza kuwa IEBC ya sasa haina nguvu.

“Kulingana na Katiba na sheria za IEBC, ni mwenyekiti wa tume tu aliye na nguvu za kufanikisha machapisho katika gazeti rasmi la serikali kwa niaba ya tume. Pia tungependa kukutaarifu kuwa, tume haimo katika nafasi nzuri ya kumteua afisa rejeshi wa kaunti atakayemkagua naibu gavana,” ilisoma sehemu ya barua ya Bw Marjan kwake Seneta Mumma.