Kisiwa cha matajiri ‘kuwafuga’ maskini

Kisiwa cha matajiri ‘kuwafuga’ maskini

Na KALUME KAZUNGU

KISIWA kidogo cha Ras Kitau katika Kaunti ya Lamu ni eneo ambalo ni vigumu mno kupata mlalahoi anayemiliki kipande hata kidogo cha ardhi.

Wengi wao ni vibarua ambao wanawafanyia matajiri kazi, ikiwemo kutunza nyumba zao za kifahari au kuchimba mawe kwenye migodi inayomilikiwa na mabwanyenye hao.Kuna watu wengine ambao ni wavuvi wa kutoka sehemu za mbali ya Lamu na hata nje, ikiwemo Malindi na Kilifi.

Wavuvi hao hupiga kambi kisiwani humo kwa muda wakijitafutia samaki na kurudi makwao kwani huwa hawadumu eneo hilo.Wakazi waliopo, ambao wengi ni vibarua, hawana vyoo, hospitali na pia mawimbi ya mawasiliano ya simu ni duni.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo ulibaini kuwa ardhi nyingi za kisiwa hicho zina hatimiliki, lakini wamiliki halisi ni mabwenyenye. Kuna wanasiasa na watalii ambao wanamiliki majumba ya kifahari eneo hilo.

Aidha, cha ajabu ni kwamba matajiri wenye mashamba na majumba eneo la Ras Kitau hawaishi eneo hilo ila wengi wao wamekita makazi yao kwenye miji kama vile Malindi, Mombasa na Nairobi.

Mabwenyenye hao huja tu Lamu kwa muda fulani, iwe ni kutazama rasilimali na mali zao eneo hilo kisha kurudi mijini.Reuben Masha ambaye ni mfanyakazi wa mmoja wa mabwanyenye eneo la Ras Kitau asema inawalazimu kuwa na uhusiano mwema na matajiri wao ili waendelee kuishi Ras Kitau.

Bw Masha asema baadhi ya matajiri wamewaruhusu kujenga nyumba za muda kwenye ardhi zao ambapo wanaishi na kufanya kazi kwenye mashamba hayo.

“Ardhi za hapa Ras Kitau zina wenyewe ambao hata wana hatimiliki. Wote ni matajiri na mlalahoi kununua ardhi hapa ni ndoto. Inatubidi kuomba matajiri wetu ruhusa kujenga vibanda vya muda kwenye ardhi zao ambavyo tunaishi tukiwafanyia kazi,” akasema Bw Masha.

Juma Kahindi asema wao hulazimika kutumia misitu badala ya vyoo kwani hawawezi kuchimba na kujenga vyoo kwenye ardhi ambazo si zao.

“Karibu sote hatuna vyoo hapa na hatuwezi kutumia vyoo vya matajiri wetu. Tunaenda msalani misituni hapa,” akasema Bw Kahidi.Bi Mary Mwangala alitaja ukosefu wa hospitali kwenye kisiwa hicho kuwa tatizo sugu linalowakosesha usingizi.

Anasema huwalazimu kusafiri kwa boti kutoka kisiwa cha Ras Kitau hadi kisiwa cha Lamu ili kutafuta matibabu wakati wanapougua.

“Sisi hulipa zaidi ya Sh2,000 kama nauli ya kusafiri kwa boti kutoka Ras Kitau hadi kwenye hospitali ya King Fahad mjini Lamu kutibiwa. Eneo la Ras Kitau halina hospitali wala zahanati. Tunaomba serikali ishughulikie suala hilo. Tunateseka,” akasisitiza Bi Mwangala.

Juhudi zetu kutafuta msimamo wa serikali ya kaunti ya Lamu kuhusu masaibu ya wakazi wa kisiwa hiki hazikufua dafu, kwani Waziri wa Ardhi, Kaunti ya Lamu, Ahmed Hemed hakupokea simu wala kujibu ujumbe aliotumiwa.

You can share this post!

BENSON MATHEKA: Wabunge wasitunge sheria kulenga mirengo ya...

Wanajeshi wakataa kupokea chanjo ya corona