Habari za Kaunti

Kisumu hatarini kupoteza hadhi takataka zikitapakaa jijini


KISUMU ipo katika hatari ya kupoteza hadhi yake kama jiji safi ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na takataka ambazo sasa zimejaa katikati mwa jiji.

Kutokana na kuzembea kwa idara ya usafi wa kaunti, wafanyabiashara, wauzaji wa vyakula katika soko la Chichwa wamekuwa wakitupa takataka katika bustani ya Jaramogi Oginga Odinga katikati mwa jiji.

Meneja anayehusika na mpangilio wa jiji Abala Wanga Jumatatu, Julai 8, 2024 alionya wanaofanya hivyo kuwa kaunti itawakabili kisheria huku akiapa watadumisha usafi nje na viungani mwa jiji hilo.

“Kuna majaa 140 ya takataka ambayo yamesambazwa ndani ya mji. Iwapo utaendelea kutupa takataka visivyo, tutakukamata na kukutoza faini kubwa,” akasema Bw Wanga.

Alikuwa akiongea wakati wa uzinduzi wa usambazaji wa majaa ya takatata katika jiji hilo na pia mitaa mbalimbali ya mabanda kama Nyalenda.

“Tutakufuatilia. Hata wale ambao wanaishi mtaa wa Nyalenda tumewaonya dhidi ya kutupa takataka katika mto Waigwa,” akaongeza Bw Wanga.

Afisa huyo wakati huohuo aliwataka wakazi wa Kisumu wawe wakipanda miti tarahe 10 kila mwezi ambapo wao pia hushiriki shughuli za kusafisha jiji hilo.