Dondoo

Kisura aaibisha kakake kutangaza alifeli KCSE

May 28th, 2018 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

BUTERE, MUMIAS

Kioja kilizuka katika eneo la hapa baada ya mzozo mkali kuzuka baina ya polo na dadake. Inadaiwa polo alitaka kumuadhibu kipusa kwa madai kwamba alimkosea heshima mbele ya marafiki zake. 

Kulingana na mdokezi, kipusa alikasirishwa na hatua ya polo kuwakaribisha marafiki zake katika chumba chake bila idhini yake.

Jamaa huyo alikuwa na mazoea ya kuwaalika marafiki katika chumba cha dada yake, jambo ambalo halikumfurahisha kipusa. Siku ya kioja demu aliamua kukomesha tabia hiyo na akamkabili mbele ya wageni.

Kipusa alianza kumfokea polo kwa kudai kwamba ni mjinga aliyefeli mitihani wa kidato cha nne (KCSE).

“Wewe ulipopelekwa shuleni ulikuwa ukiongoza kutokea nyuma. Ungekuwa na akili nzuri hungewaleta hawa watu kwa nyumba yangu.

Kuwa na heshima,” kipusa alimwambia polo. Duru zinasema baada ya marafiki zake kuondoka, polo aliamua kumvamia dadake huku akiapa kumpa adabu. Inasemekana ilikuwa ni hali ya miguu niponye kwa kipusa.

“Huwezi kuniaibisha hivyo mbele ya marafiki zangu. Hata kama nilianguka shuleni, wewe ni mtoto sana kunitusi,” polo alimkaripia dadake.  Majirani walibaki kutazama sinema ya bure.

“Kwenda kabisa. Ukitaka kuolewa nenda ukaolewe. Sijui unafanya nini hapa,” polo alimkemea kipusa.

Hata hivyo mwanadada aliapa kutokubali jamaa kuwakaribisha wageni wake katika chumba chake.

“Ni kweli ulifeli mtihani kwa sababu ya tabia kama hii. Hauna haya kualika marafiki katika nyumba ya dada yako hata siwezi kupata nafasi ya kufanya kazi zangu. Bure kabisa wewe,” demu aliwaka.

Majirani walimuunga mkono na kumlaumu jamaa kwa kukosa heshima. Walimsaidia mwanadada kumfukuza jamaa wakisema hawangetazama akimdhulumu dada yake.

…WAZO BONZO…