Kimataifa

Kisura agundua ni mjamzito baada ya kumtema mumewe wa wiki moja

January 21st, 2020 1 min read

MASHIRIKA na MARY WANGARI

MWANAMITINDO wa Japan aliyemtaliki mumewe majuzi waliyeoana kwa wiki moja baada ya kutumia hela zake za Sh1.2 bilioni sasa ni mjamzito.

Katika video iliyochapishwa mnamo Jumatatu, Januari 19, 2020, Kato aliomba radhi kwa video iliyokuwa imetolewa awali pamoja na mpigapicha wake ambaye jina lake halikutambulishwa.

Katika video hiyo, Kato alikuwa ndio mwanzo tu amefahamu kwamba ni mjamzito.

Mpigapicha huyo alizomewa vikali kwa sababu alionekana kuchukulia kiholela habari za ujauzito wake na kumuuliza mara kwa mara maswali nyeti.

Wanamitandao wengi walihisi kwamba hakuwa na utu hasa katika kipindi hicho kigumu kwake.

Video hiyo ilirekodiwa baada ya wawili hao kuelekea katika kliniki ya upasuaji wa urembo, ambapo tabibu alithibitisha kwamba Kato hakufanyiwa upasuaji wowote wa urembo usoni mwake au kwenye matiti yake.

Wakati daktari huyo alisema inawezekana kwa wanawake wajawazito kuwa na maziwa makubwa, Kato alidokeza kwamba hajapokea hedhi yake kwa miezi minne iliyopita.

Hapo ndipo alifanyiwa vipimo hospitalini humo siku tofauti ambapo aligunduliwa kuwa na mimba.

Kato hakufichua ni nani baba ya mtoto wake na hata akaonekana kukosa uhakika kuhusu anayeweza kuwa amempa mimba.

Hata hivyo, alikuwa imara katika uamuzi wake wa kujifungua mtoto wake na hata kumlea akiwa pekee yake.

Katika video hiyo ya kuomba msamaha, Kato aliomba radhi kwa hisia hasi kutokana na video ya awali.

Aidha, aliomba radhi kwa niaba ya mpiga picha yake na kuahidi kutorudia kosa kama hilo katika video za siku zijazo.

Licha ya kuomba msamaha, wanamitandao nchini Japan bado hawakuridhika kwamba ndiye aliyeomba msamaha badala ya mpiga picha wake, waliyemwona na makosa.

Lakini tofauti na shutuma kali ambazo Kato alipokea katika video alipofichua kumtaliki mumewe baada ya kumweleza apunguze matumizi, wanamitandao wengi walimuunga mkono.