Dondoo

Kisura ajuta panya kutafuna maelfu aliyopora mumewe

March 14th, 2019 1 min read

Na Ludovick Mbogholi

KIMBUNGA-KASHANI, MOMBASA

MREMBO aliyezoea kumpora mumewe maelfu ya pesa na kuzificha chini ya godoro alijipata pabaya baada ya hila zake kubainika, panya walipomsababishia hasara.

Inasemekana mwanadada alienda kwao kuomboleza na aliporudi, alishtuka kuona godoro lilikuwa limetafunwa na panya pamoja na bunda la noti alizokuwa ameficha chini yake. Kulingana na mdokezi, mumewe alikuwa safarini wakati huo.

“Mwanadada alirejea kutoka kwao, akapekua godoro na kupata vipande vidogodogo vya noti alizokuwa ameficha na akahuzunika zaidi,” alidokeza mdaku wetu.

Inasemekana mwanadada huyo alikuwa akimwitisha mumewe hela za matumizi na kuzificha akisingizia zilikuwa zimeisha. “Kila akipewa pesa za matumizi alikuwa akizibana na kuitisha zingine,” mdokezi anayefahamu tabia ya mwanadada alisema.

Duru zinasema mumewe alifika na kumpata akiwa amenuna na kumuuliza kilichokuwa kimejiri.

“Mumewe aliporudi alimkuta kanuna huku akijipangusa machozi, alimuuliza sababu ya kulia naye akashindwa kumweleza,” alisimulia mdokezi.

Lakini mume alipokuwa akimbembeleza, alishangaa kuona vipande vya noti za elfu moja vikipeperushwa na upepo kutoka chini ya kitanda chake na kumuuliza vilitoka wapi.

“Hivi vipande vya noti vinatoka wapi chini ya kitanda,” mumewe alimuuliza mkewe kwa mshangao. Mrembo alitulia kisha akaanza kusimulia.

“Kumbe wewe mwanamke mbaya namna hii, bahili mkubwa usiye na haya, nikikupa pesa unaficha chini ya godoro halafu unasema zimeisha nikupe zingine,” alifoka polo huku akitetemeka mwilini kwa hasira.

“Nisamehe, sikukusudia mabaya, nilizihifadhi zitusaidie ukiishiwa,” mwanadada alijitetea. Polo huyo ambaye alioa miezi kumi iliyopita hakumsikiliza.

“Siwezi kuishi na mwanamke sampuli yako. Yaani Sh10,000 unawalisha panya? Kesho utarudi kwenu,” jamaa aliropokwa huku akisonya kwa hasira.